Na James K. Mwanamyoto-Rufiji
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezitaka Taasisi za Umma nchini kuzingatia Sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 ya Mwaka 2019 na Kanuni zake za Mwaka 2020 pindi zinapotaka kuanzisha mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma kwa wananchi ili mifumo hiyo iweze kuongeza ufanisi kiutendaji na kuleta tija katika maendeleo ya taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi wa Rufiji mara baada ya Mwenge wa Uhuru kupokelewa Wilayani humo kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kutoa ujumbe wake wa mwaka huu unaosisitiza matumizi mazuri ya TEHAMA kwa wananchi na kwenye Taasisi za Umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa na Mwenge wa Uhuru mara baada ya Mwenge huo kupokelewa Wilayani Rufiji.
Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 Luteni Josephine Mwambashi akizungumza na wananchi wa Rufiji (hawapo pichani) mara baada ya Mwenge wa Uhuru kupokelewa Wilayani humo kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kutoa ujumbe wake wa mwaka huu kwa wananchi wilayani humo.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo Wilayani Rufiji akiwa ni Waziri mwenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) mara baada ya Mwenge wa Uhuru kupokelewa Wilayani humo kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kutoa ujumbe wake wa mwaka huu ambao unasisitiza matumizi mazuri ya TEHAMA kwa wananchi na kwenye Taasisi za Umma.
Akizungumzia utekelezaji wa kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021, Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali kwa upande wake imepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa kuziunganisha taasisi zake kwenye mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma, hivyo ujumbe wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka huu unaosisitiza matumizi sahihi kwenye eneo la uwajibikaji umetekelezwa kikamilifu na Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Meja Edward Gowelle akimtambulisha Balozi wa Mapambano dhidi ya rushwa Mzee Yusuph Mpili mara baada ya Mwenge wa Uhuru kupokelewa Wilayani humo kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kutoa ujumbe wake wa mwaka huu kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Amesisitiza kuwa, Serikali inaunga mkono ujumbe wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ambao umelenga kuhimiza uwajibikaji kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwasababu moja ya lengo lake ni kukagua miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mwenge wa uhuru unapopita na kukagua miradi ya maendeleo unaacha alama na kutoa maagizo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Ili kuhakikisha kuna matumizi mazuri ya fedha za miradi zinazotolewa na Serikali, Mhe. Mchengerwa ameielekeza TAKUKURU kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu ili kujiridhisha kama zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishiriki kukimbiza Mwenge wa Uhuru na viongozi wengine mara baada ya Mwenge huo wa Uhuru kuwasili Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Balozi wa Mapambano dhidi ya rushwa Mzee Yusuph Mpili kwenye banda la Klabu ya Wapinga Rushwa la Shule ya Sekondari Ikwiriri mara baada ya waziri huyo kutembelea banda hilo ili kupata maelezo ya namna klabu hiyo inashiriki mapambo ya dhidi ya rushwa.
“Fedha zinazotolewa ni za umma na zinatokana na kodi za wananchi hivyo ni lazima Taasisi zinazohusika kusimamia matumizi ya fedha za umma zitekeleze wajibu wake ili kuondoa ubadhilifu na kuwawezesha wananchi kufaidi matunda ya miradi inayotekelezwa na Serikali,” Mhe. amesisitiza.
Ameongeza kuwa, watumishi wa TAKUKURU kuanzia ngazi ya taifa hadi wilaya wanapaswa kufanya ufuatiliaji kujiridhisha kama wakandarasi waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya maendeleo wanazo sifa na vigezo stahiki vya kuitekeleza miradi hiyo kwa ufanisi ili wananchi wanufaike na miradi hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Meja Edward Gowelle amesema Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu zimetoa funzo la namna wananchi wanapaswa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akielezwa jambo na Balozi wa Mapambano dhidi ya rushwa Mzee Yusuph Mpili kwenye banda la Klabu ya Wapinga Rushwa la Shule ya Sekondari Ikwiriri mara baada ya waziri huyo kutembelea banda hilo ili kupata maelezo ya namna klabu hiyo inashiriki mapambo ya dhidi ya rushwa.
Sanjari na hilo, amesema wilaya yake imejifunza namna Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo wanavyopaswa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo yeye kama kiongozi na msimamizi mkuu wa miradi kwenye wilaya yake atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kusimamia miradi hiyo ambayo Serikali imetumia fedha nyingi kuanzisha miradi hiyo.
Kaulimbiu ya Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 inasema “TEHAMA NI MSINGI WA TAIFA ENDELEVU, ITUMIKE KWA USAHIHI NA UWAJIBIKAJI”, hivyo ni jukumu la kila mtanzania na Taasisi za Umma kuunga mkono matumizi sahihi ya TEMAHA kwa maendeleo ya Taifa.