*Awahamasisha wananchi waongeze mashamba, parachichi zina faida kubwa
NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea shamba la parachichi na kiwanda cha kuchakata mazao ya parachichi na kuwasisitiza wananchi walime zao hilo kwa kuwa faida yake ni kubwa.
Ametembelea shamba hilo leo Jumapili, Agosti 1, 2021. Shamba lipo katika kijiji cha Ilolo wilaya ya Rungwe, Mbeya na linamilikiwa na kampuni ya Kuza Africa na Moravian Farming PVT.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mtambo wa kuchakata parachichi wakati alipotembelea shamba la kiwanda cha Kampuni ya Kuza Afrika Limited lililopo Kikota Rungwe, Agosti 1, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Kilimo cha parachichi kina manufaa makubwa sana, wananchi ongezeni ukubwa wa mashamba ya parachichi na Serikali italisimamia kuanzia hatua za maandalizi ya shamba hadi masoko.”
Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote zinazolima zao la parachichi zianzishe vitalu vya kuotesha miche na kuigawa kwa wakulima ili kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo.
Amesema zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa kwa gharama nafuu, hivyo amewahimiza wananchi kulima zao hilo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama shamba la parachichi la Kampuni ya Kuza Afrika Limited ya Kikota Rungwe, Agosti 1, 2021. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na wa tatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Naye, Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewapongeza wawekezaji hao kwa kuwa wamewezesha wakulima kutatua changamoto ya soko la uhakika wa zao la parachichi.
Naibu Waziri huyo amesema mbali na kupatikana kwa soko la parachichi katika kiwanda hicho pia Serikali itahakikisha soko la parachichi za Tanzania nchini Afrika Kusini linafunguliwa.
Awali, Meneja Rasilimali Watu wa kampuni hizo Noel Kabuje alisema wamewezesha wakulima kupata soko la uhakika la parachichi kupitia ununuzi wa matunda ya parachichi kutoka kwao.
Shamba la parachichi la Kampuni ya Kuza Afrika Limited ya Kikota Rungwe ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilitembelea Agosti 1, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Mbali na kulima parachichi sisi wenyewe pia tunanunua matunda ya parachichi kutoka kwa wakulima wadogo, tunayachakata na kufungasha matunda ya parachichi na kuyauza nje.”
Meneja huyo alisema mbali na kusafirisha parachichi pia kampuni yao inauza mbegu za matunda ya parachichi zitokanazo na miparachichi ya asili (kienyeji) kwenye soko la dunia.
Alisema kwa sasa kampuni yao imeanza kupanda parachichi za kisasa (Hass Avocado) kwenye mashamba yao pamoja na kwenye mashamba ya wakulima wakubwa na wadogo.
Alisema mbali na kuwapandia miche hiyo ya kisasa pia inatoa huduma za ugani na pembejeo kwa wakulima. “Tumeshawafikia wakulima zaidi ya 10,000 ambao tumewapa miche ya kisasa.”
Meneja huyo alisema kwa sasa masoko ya parachichi yameongezeka ambapo wanauza katika nchi za Ujerumani, Italia, Ufaransa, Mashariki ya Kati, Uingereza na Hong Kong.
Tags
Habari