NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 50 kwenye Bajeti ya mwaka 2021/22 kwa ajili ya kununua vitabu vya kiada kwa wanafunzi wote wa msingi na sekondari nchini.
Mhshimiwa Ummy amesema, upatikanaji wa vitabu hivyo utapelekea kila mwanafunzi kupata kitabu chake mwenyewe sawa na muongozo unavyotaka wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja yaani 1:1.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo alipokua akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bugumbikiso Kata ya Chifunfu Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza walipolalamikia uhaba wa vitabu shuleni hapo.