NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT- Wazalendo Mhe. Othman Masoud Othman, amesema Zanzibar inayo fursa kubwa ya maendeleo na kuondoa umasikini, bali inahitaji viongozi makini na waadilifu wenye upeo wa mbali wa kuongoza katika kuikwamua kiuchumi.
Amesema viongozi hao ni wale wenye moyo wa kuutumikia umma, msimamo thabiti na nia ya dhati ya kupambana na matatizo ya kijamii, watakaokabiliana na tatizo sugu la ukosefu wa ajira na hatimaye kuondoa umasikini nchini.
Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo huko Kianga Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja alipofungua Mkutano Mkuu wa Mkoa Magharib ‘A’ kichama, wa Chama hicho.
Amefahamisha kuwa Zanzibar hivi sasa ina vijana wengi waliohitimu elimu za viwango vya juu, lakini wanavunjika moyo kutokana na ukosefu wa ajira, huku wakiendelea kusotea maisha ya kubabaisha.
Ametaja kuwa hali hiyo imetokana na baadhi ya viongozi waliokosa uadilifu kwa umma, ambapo wengi katika upeo wao unaangaza kujipatia maslahi binafsi na siyo maendeleo ya nchi.
Akitolea mfano baadhi ya nchi ambazo kijografia zinalingana na visiwa vya Unguja na Pemba Mhe. Othman alisema, “ sisi ni wachache sana lakini tunashindwa na nchi kama Seychelles, Singapore, nazo ni nchi ndogo sana mfano wa kisiwa cha Tumbatu, lakini kutokana umakini wao na viongozi wameweza kupiga hatua”.
“Kiongozi mwenye imani na anayefuata vyema misingi ya uadilifu husaidia sana nchi kuwa na amani na maendeleo”, alifahamisha.
Aliwataka viongozi hao kuendelea kujitolea kukitumikia chama chao kwani ndio mtaji mkubwa na muhimu utakaowawezesha kuendelea kupata viongozi bora katika ngazi mbali mbali.
Akiweka msisitizo juu ya haja ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar alisema, “msikubali kubabaishwa , madhumuni yake makubwa ni kujenga nchi kwa pamoja na hiyo ni katika siri ya mafanikio ya nchi mbali mbali kama vile Uengereza, Ujerumani, Palestina , Israel, India na Italia, wao hawaamini kabisa kwamba nchi inaweza kuendeshwa kwa chama kimoja”.
Naye Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo wa Mkoa huo Raisa Abdalla Mussa aliwahimiza viongozi hao kushiriki vyema katika vikao vya Chama ili kuendeleza ufanisi na uhai wa chama.