NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe ameweka wazi kuwa ikitokea akapata uteuzi wa nyadhifa serikalini kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, hataweza kuafiki kwani kwa sasa ameweka nguvu na maono yake kwenye kujenga chama kwanza.
Zitto amebainisha hayo kwenye mahojiano yaliyofanyika na kituo cha televisheni cha Star Tv siku ya Jumamosi usiku ambapo mtangazaji alimuuliza ikiwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan atamteua na kumpa nafasi kama ilivyokuwa kwa mmoja wa aliyekuwa mshauri wa chama cha ACT Wazalendo Dkt. Kitila Mkumbo, aliyepata uteuzi wa Rais aliyepita Hayati Dkt. Joseph Magufuli.
Akijibu swali hilo, Zitto alisema, “hapana nataka nijenge chama, huwezi kujenga taifa ukiwa na vyama goigoi, lazima uimarishe vyama vya siasa ili uwe na vyama madhubuti, vizae serikali madhubuti, kwa sasa hivi naona utume wangu sio kuwa serikalini, utume wangu ni kuijenga ACT kiweze kuwa chama imara ambacho kina weza kudhibiti mapigo ya aina yoyote na kinachoweza kuzalisha serikali itayoweza kuhudumia watanzania vizuri.
"Nitamshukuru Rais kwa imani yake kwangu ila nitamuomba atafute mtu mwingine atakayeweza kuifanya kazi ambayo mimi ningeweza kuifanya ili mimi nipate nafasi ya kuweza kujenga chama cha ACT Wazalendo,"amesema Mheshimiwa Zitto.
Akizungumzia uchaguzi mkuu wa 2020, ambao ripoti yake ilipokelewa Jumamosi na Rais Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Tume ya Uchaguzi, Zitto alisema katika hali halisi hapakuwa na uchaguzi bali operesheni ya kuturudisha kwenye mfumo wa chama kimoja.
Aliongeza kuwa hii ndio sababu viongozi wengi mahiri wa upinzani wenye uwezo wa kujenga hoja bungeni waliondolewa.
“Binafsi sikushindwa uchaguzi wowote halali Kigoma, nimefanya kazi kubwa sana Kigoma kipindi chote nilichokuwa kwenye siasa na nimepandisha hadhi ya Mkoa wa Kigoma, uchaguzi ulikuwa mbovu, sio kwamba wana Kigoma walinikataa,” alisema Zitto, akiongeza kuwa, anaamini kuwa wapo wana CCM wenye uwezo mkubwa ambao wangeshinda kihalali vilevile kama uchaguzi usingevurugwa.
Akijibu swali kuhusu tofauti ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na utawala uliopita, Zitto alisema kuna baadhi ya mambo Mheshimiwa Rais amebadilisha akatolea mfano uhuru wa vyombo vya habari.
Wakati huo huo Zitto aliongeza kuwa, kuna baadhi ya mambo ambayo taifa lilitegemea yabadilike ila bado yanaonekana.
“Kwa mfano kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wanachama wa Chadema Mwanza na mmoja wa kiongozi wetu, mpaka sasa siamini kama kulikuwa na sababu ya kumkamata Mbowe na kumuweka ndani mpaka sasa,”alisema.
Aliongeza kuwa, hawezi kuzungumzia kwa undani suala la Mbowe ila kimsingi kesi inatakiwa iwe ni mihimili mikuu miwili ambayo ni ushahidi wa kesi, na maslahi ya taifa.
"Vitu ambayo kwa maono yangu, kesi ya Mbowe haina, na hata kama kuna ushaidi, sioni maslahi ya taifa zaidi ya kuligawa taifa,”amesema.
Aliongeza kuwa, kuna umuhimu wa vyama vya siasa kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan kujadili namna ya kufanya siasa za hoja ili tuwe na muelekeo mzuri nchini.
MUHIMU
UNATAMANI DIRAMAKINI BLOG TUWE HEWANI SAA 24 KUKUPA HABARI ZA KINA KILA DAKIKA, TUNAOMBA UTUUNGE MKONO KWA KUCHANGIA GHARAMA ZA MAWASILIANO NA INTANETI KWA WAANDISHI WETU POPOTE WALIPO NDANI NA NJE YA TANZANIA; TUNAPOKEA MCHANGO WAKO KUPITIA 0719254464 (Tigo Pesa-Godfrey Nnko) AU UKIHITAJI NAMBA YA BENKI TUJULISHE. MUNGU AKUBARIKI SANA KWA SAPOTI YAKO. ASANTE