Hawa ndiyo Askari Saba wa Polisi Tanzania waliofukuzwa kazi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewafukuza kazi askari saba wa Kituo cha Polisi wilayani Ileje.
Ni askari ambao wanadaiwa kuingia na kufanya kazi ya kufukuzia magendo nchi jirani ya Malawi bila kuwa na kibali cha Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) na kutaka kusababisha uhusiano kati ya Tanzania na Malawi kutetereka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi amesema kuwa, askari hao walitenda makosa hayo Septemba 15, mwaka huu, majira ya kati ya saa 10:00 hadi saa 12:45 jioni ambapo walikiuka miongozo na misingi inayoongoza jeshi hilo (PGO) na kwenda kukamata magendo katika nchi jirani ya Malawi.

Kamanda amesema kuwa,askari hao walitenda makosa hayo ya utovu wa nidhamu kwa kuingia na kwenda kufanya kazi nchi jirani ya Malawi bila kuwa na kibali cha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), huku wakiwa na bunduki mbili aina ya SMG kila moja ikiwa na risasi 30 hali ambayo imelidhalilisha jeshi la polisi na kuifedhehesha nchi.

“Askari hawa wamefukuzwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu ambapo Septemba 15, mwaka huu waliingia nchi jirani ya Malawi katika Wilaya ya Chitipa na kwenda kufanya kazi ya kukamata magendo bila kutoa taarifa yeyote kinyume na miongozo na taratibu za jeshi la polisi,”amesema Kamanda Magomi.

Askari waliofukuzwa kazi ni Sajenti Ramadhan, Pc Jumanne, Pc Joseph, Pc Husein, Pc Edward, Pc Safari pamoja na Wp Anastazia.

Inadaiwa kuwa, Septemba 15 mwaka huu katika Kitongoji cha Mtima katika Kijiji cha Ikumbilo Kata ya Chitete, Tarafa ya Bulambya, wilaya ya Ileje, askari mpelelezi mwenye namba G.3695 Ramadhani ambaye ni kiongozi wa askari wenzake sita, Pc Edward, Pc Safari, Wp Anastazia, Pc Joseph, Pc Hussein, Pc Jumanne wakiwa na gari lenye namba PT.3676 Toyota Cruiser mali ya jeshi la polisi Tanzania wakiwa katika Kijiji cha Mtima waliona pikipiki inayosadikiwa kuwa imebeba magendo kutoka nchi jirani ya Malawi, waliisimamisha lakini pikipiki hiyo iliamua kukimbia kuelekea nchi jirani ya Malawi.

Akari hao, inadaiwa waliamua kuifukuzia na kuvuka mpaka wa Tanzania na kuingia nchini Malawi na ndipo wananchi wa Malawi walilizingira gari hilo likiwa na askari hao na kuanza kuwashambulia kwa mawe kabla ya kuokolewa na askari wa nchi hiyo ya Malawi.

Askari Ramadhani ambaye alikuwa kiongozi wao, Pc Safari na Pc 9727 Joseph walifanikiwa kutoroka katika vurugu hizo na kurudi kituoni salama.

Kwa nyakati tofauti wananchi wa mjini Ileje wameieleza DIRAMAKINI Blog kuwa, uamuzi huo wa Jeshi la Polisi ni sahihi na unapaswa kuwa fundisho kwa maafisa wengine waliopewa jukumu la kusimamia taasisi mbalimbali za umma.

"Kwa ufahamu wangu mdogo ni jambo lisilowezekana askari mwenye silaha kuingia nchi jirani au nyingine eti kwa madai ya kufuatilia magendo, huo ni ugomvi mkubwa, jambo kama lile limeonyesha udhaifu miongoni mwetu, yafaa sana wenye mamlaka waangalie namna ya kuteta na ndugu zetu ili kulimaliza jambo hilo kiutu uzima,"amesema Amos mkazi wa Ileje katika mazungumzo na DIRAMAKINI Blog.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news