Benki ya Stanbic yaunga mkono Sekta ya Elimu nchini

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Benki ya Stanbic imeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha Sekta ya Elimu nchini kwa kutoa madawati na viti 100 katika Shule ya Sekondari Mbabala jijini Dodoma vyenye thamani ya shilingi milioni 12.

Akikabidhi madawati hayo mbele ya uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkurugenzi wa benki hiyo ya Stanbic, Omary Kitiga amesema, zoezi hilo limeanza rasmi baada ya kuzindua kampeni yao iliyozinduliwa hivi karibu jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako.

Omary amesema kuwa, wamejikita kwenye meza na viti baada ya kuongea na wizara husika na kubaini uhitaji wa madawati ni mkubwa na kupitia vifaa hivyo vitaenda kusaidia kuboresha elimu zaidi hapa nchini ambavyo Serikali ina nia ya kuboresha elimu.

Amesema kuwa, mbali na msaada huo wamedhamiria kupanda miti 100 kwa ajili ya kuuwisha mazingira ikiwa ni dhana yao kwamba dawati moja ni sawa na mti mmoja jambo ambalo litasaidia kuendelea kutunza ,kulinda na kuboresha mazingira.

"Benki yetu ya Stanbic leo tumeanza zoezi hili la kugawa madawati na viti miamoja tukianza na makao makuu ya nchi na lengo ni kugawa vifaa hivyo nchi nzima ambapo kwa mwaka tumekusudia kugawa madawati 1000, japo wakati tukizindua kampeni hii kulijitokeza mdau ambaye alichangia mengine 1000, hivyo jumla tutagawa madawati na viti 2000,"amesema Omary.

Ameongeza kuwa, Benki ya Stanbic imekuwepo kwa zaidi ya miaka 20 ambapo makao makuu yako jijini Dar es Salaam huku ikiwa na matawi mikoa ya Mwanza, Arusha,Kilimanjaro,Mbeya Dodoma na hata sehemu ambazo sio rasmi ambapo huwa wanatoa huduma kwa njia ya kidijitali na kielektroniki.

"Katika kuchangia kiuchumi tumeaajiri zaidi ya Watanzania 500 hapa nchi na benki yetu imekuwa ikichangia na kuwezesha miradi mikubwa ya Serikali ambapo mwaka jana ilitolewa sh.bilioni 300 kwa ajili ya shughuli za kiuchumi,kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama reli,barabara na kuwawezesha makandarasi,"amesema.

Mbali na hayo amesema, benki imezindua dawati maalumu kwa ajili ya kilimo biashara ili kuongeza ufanisi na kumsaidia mkulima apate tija zaidi.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amesema, benki ya Stanbic wamefanya jambo jema na wameona umuhimu kuwekeza kwenye elimu jambo ambalo litasaidia kutatua changomoto ya madawati ukizingatia kwa sasa Jiji la Dodoma lina ongezeko la wanafunzi kutokana na kuwepo kwa makao makuu.

"Tunaomba ushirikiano huu uendelee na ningeomba shule hiyo muichukue ili iwe shule ya mfano kila mtu atakae fika hapo aone mliyoyafanya, lakini pia bado tunahitaji kompyuta kwa ajili ya kuchapisha mitihani ya kila wiki, tunaomba mtusaidie,"amesema.

Afisa Elimu, Vifaa na Takwimu, Fredrick Mwakisambwe alisema kuwa, benki hiyo ya Stanbic imefanya jambo kubwa sana kutokana na Jiji la Dodoma kukabiliwa na uhaba wa madawati na viti.

Amesema, hapo awali walikuwa na uhitaji wa vifaa hivyo 7,000, halmashauri inaendelea na jitihada kumaliza changamoto na kwamba hiyo benki imeleta chachu katika sekta ya elimu.

Awali akiongea katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema, benki hiyo imeunga jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan mkono kutaka kuboresha Sekta ya Elimu hapa nchini ambapo aliwataka wanafunzi kutunza madawati hayo, kwani wamepewa madawati kwa lengo la kufanya vizuri kimasomo na siyo kuyaharibu.

Amesema, wanapoelekea kufanya mitihani yao wazingatie masomo vizuri na wafanye mazoezi kwa sana na kuwataka wazazi wasimamie watoto ikiwemo kutoa nafasi sawa bila kujali jinsia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news