NA GODFREY NNKO
Baada ya Klabu ya Simba yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi chini ya Bilionea Mohamed Dewji,kuendelea kuchechemea kwa kupoteza mechi tatu mfululizo kwa siku za karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji ametangaza kujiuzulu.
Vijana wa Msimbazi walianza kupoteza kuanzia mechi ya Simba Day waliofungwa bao 1-0 na TP Mazembe, mechi ya Yanga ya Ngao ya Jamii ambapo Simba aliambulia kichapo cha bao 1-0 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Aidha, jana huko Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Biashara United katika mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara, waliwadhibiti.
MO Dewji ambaye anamiliki asilimia 49 ya hisa za Simba SC kwa thamani ya sh.Bilioni 20 ametangaza leo rasmi kujiuzulu nafasi yake Uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ndani ya Simba SC.
Aidha,nafasi yake itachukuliwa na aliyekuwa Makamu wake, Salim Abdallah (Try Again), MO Dewji amefikia uamuzi huo kutokana na mara nyingi kutokuwa nchini.
“Mmetuunga mkono kwa miaka minne ya Uongozi wangu kama Mwenyekiti wa Bodi, kwenye miaka minne tumepata mafanikio makubwa tumeshinda Ligi mara 4 na kufanya vizuri kwenye Champions League muda umefika kama Mohammed na tumekubaliana mimi nitajiuzulu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba SC naomba sana msifikie kuwa Mimi nimeondoka Simba bali bado ni Muwekezaji,”amesema.