Na Robert Kalokola,Geita
Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Dhahabu ya Buckreef Gold Company Limited imesema itaungana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule katika kampeni yake ya siku tatu za kuongoza wanawake kuchangia damu katika Maonesho ya Dhahabu katika viwanja vya EPZA mjini Geita.
Afisa Rasilimali Watu, Emarda Msuya (wa kwanza kulia) akizungumzia ushiriki wa kampuni hiyo katika kuchangia damu katika maonesho ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Hayo yamesemwa na Afisa Raslimali Watu wa Buckreef Gold Company Limited, Emarda Msuya katika Maonesho ya Uwekezaji na Teknolojia ya Uchimbaji katika Sekta Madini mjini Geita ambapo mgodi huo umeshiriki maonesho hayo.
Msuya ameongeza kuwa, kwa kutambua kuwa wanawake wengi wanapoteza maisha wakati wa kujifungua kwa kukosa damu salama yeye pamoja na wafanyakazi wenzake wa Buckreef wataungana na mkuu wa mkoa wa Geita kuchangia damu kwa hiari.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ametangaza siku tatu kuanzia Septemba 23 hadi Septemba 25, mwaka huu kuwa ni siku tatu za wanawake katika Mkoa wa Geita kujitokeza kwa hiari kuchangia damu katika banda la damu salama ambalo linaratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Geita kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Idara ya Afya.
Mtaalam kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita Kitengo cha Damu Salama, Magidalena Gumbu amesema, hospitali hiyo ina akiba ya uniti 150 ambazo hazitoshi mwezi mzima huku mahitaji ya mwezi mmoja ni uniti 600.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akiwa katika viwanja vya EPZA mjini Geita kwenye maonesho ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini baada ya kutembelea Banda la Buckreef Gold Company Limited. (Picha na Robert Kalokola).
Ili kukabiliana na upungufu huo Chama cha Waandishi wa Habari mji wa Geita (GMG) kwa kushirikiana na Idara ya Afya mkoa wa Geita kimeandaa kazi ya siku kumi kukusanya damu salama kwa watu wanaofika kwa hiari kujitolea damu katika banda maalum katika maonyesho ya uwekezaji na teknolijia ya dhahabu mjini Geita.
Makamu Mweneyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mji wa Geita, Mutta Robert amesema kuwa, chama hicho killishirikisha wadau mbalimbali kuchangia gharama za ukusanyaji wa damu salama ili kuweza kukabiliana na upungufu wa damu salama katika Hospitali ya Rufaa na kuokoa maisha ya wanawake wanaojifungua,watoto na wagonjwa wengine.
Aidha, Afisa Raslimali watu Emarda Msuya ameongeza kuwa kampuni hiyo ya Buckreef Gold Company Limited imeamua kushiriki maonesho hayo ya uwekezaji ili jamii iweze kutambua kazi zinazofanywa na kampuni hiyo katika shughuli zao za kila siku.
Amesema kuwa mgodi huo umeshachangia madawati zaidi ya 300 kwa ajili ya wanafunzi shuleni pamoja na kujenga vyumba vinne vya madarasa kwa shule ili kuunga mkono jitihadi za serikali katika sekta ya elimu.