NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro, kimesema maamuzi yaliyofanywa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zefrin Lubuva ya kuzuia magari mawili ya mkandarasi kutoka Kampuni ya Bona and Hubert Engineering (T) Ltd anayejenga kipande cha barabara ya Mwanga-Kikweni-Vuchama, zaidi ya kilomita 4.2 kwa kiwango cha lami ni batili.
Mwenyekiti wa chama hicho mkoa, Patrick Boisafi ameyasema hayo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa kilichokaa mjini Moshi.
Amesema, maamuzi yaliyochukuliwa na mkurugenzi huyo, ni yake binafsi na sio mambo ya kiutumishi na chama hakitakubaliana na mamauzi hayo.
Mheshimiwa Boisafi amesema, kitendo hicho kimeisababishia Serikali kupata hasara, hivyo CCM haipo tayari kuona Serikali inaingiziwa hasara kwa mambo ambayo hayana tija kwa wananchi.
Aidha,kufuatia hali hiyo, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wamepitisha kwa kauli moja, magari yaliyokamatwa ya mkandarasi huyo kuachiwa na ujenzi wa barabara hiyo uendelee na ukamilike kwa wakati ili kunufaisha wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai akizungumzia tukio hilo amesema, alishatoa maelekezo magari hayo yaachiliwe bila kutekelezwa na kumuagiza katibu tawala wa mkoa huo, Dkt. Seif Shekalaghe, kufuatilia na iwapo kutakuwa na hasara yoyote iliyopatikana kutokana na kukamatwa kwa magari hayo, Mkurugenzi huyo awajibike.
Mwezi Agosti ,2018, Lubuva alikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Golden A. Mgonzo.
Makabidhiano hayo yalifanyikia kwenye ukumbi wa TRC-Mwanga ambapo Mgonzo alitoa shukrani za dhati kwa watumishi wote kwa namna walivyompa ushirikiano kipindi chake chote cha uongozi wilayani Mwanga huku akimshauri Mkurugenzi aliyechukua nafasi yake kuhakikisha kuwa, anasimamia vizuri mapato ya Halmashauri.
Alisema kuwa Halmashauri ina vyanzo vingi vya mapato hivyo ni vyema vikasimamiwa vizuri.