Na Yusuph Mussa, Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwenda kuchunguza matumizi ya fedha za ujenzi wa nyumba ya mwalimu yenye uwezo wa kuishi familia mbili (Two in one) iliyopo Shule ya Msingi Kwaboli iliyopo Kijiji cha Migambo.
Ni baada ya kufika kwenye shule hiyo Septemba 28, 2021 kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi, ambapo alielezwa kuwa nyumba hiyo ambayo ilijengwa kwa nguvu za wananchi hadi usawa wa linta, lakini kwenye ukamilishaji wa kuweka linta hadi kupaua, huku upande mmoja wa nyumba ukiwa umekamilika ulitumia sh. milioni 25.
Lazaro alihoji matumizi hayo yanahitaji kuchunguzwa kwa madai tayari kazi kubwa ilifanywa na wananchi, hivyo haiwezekani kutumia kiasi hicho cha pesa, huku upande mmoja wa jengo hilo ukiwa bado haujakamilika.
"Ili kuondoa utata, naagiza TAKUKURU waje kuchunguza fedha iliyotumika hadi sasa kwenye ujenzi huu. Jana (Septemba 27) nimekwenda Shule ya Msingi Mbula, nimekuta wamejenga madarasa mawili na darasa moja likiwa limepauliwa, lakini wametumia sh. milioni 12. Itakuwaje hapa watumie sh. milioni 25 bila kukamilisha nyumba hii ya walimu,"amesema Lazaro.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi 'Bosnia' alimuomba Mkuu wa Wilaya jambo hilo amueleze Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima atume Timu ya Ukaguzi kutoka mkoani ili kujua ukweli wa jambo hilo, sababu thamani ya fedha haina uhalisia.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Emmanuel Vuri alimueleza Mkuu wa Wilaya kuwa tayari TAKUKURU wanachunguza jambo hilo, kwani Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (FUM) Juni, mwaka huu, ilituma wataalamu kuchunguza suala hilo, na walipobaini kuna mashaka ya matumizi ya fedha, Kamati iliiagiza TAKUKURU kwenda kuchunguza.
"Mkuu, tayari jambo hili lipo TAKUKURU, na wanaendelea na uchunguzi wao. Ni baada ya Kamati ya Fedha kutuma wataalamu wake, na kubaini kunahitajika uchunguzi ili kubaini matumizi halisi ya fedha sh. milioni 25,"amesema Vuri.
Akihutubia mkutano wa hadhara Kata ya Migambo, Lazaro aliagiza kutolewa kwa watu wote wanaofanya shughuli zao kwenye chanzo cha maji kilichopo Kitongoji cha Kwaboli, kwani jitihada zinazofanywa na Serikali kupeleka fedha za miradi ya maji kwenye ngazi ya kata, vijiji na vitongoji itakuwa haina faida kama wananchi wataharibu vyanzo vya maji.
"Naagiza huyo aliyevamia chanzo cha maji Kitongoji cha Kwaboli aondoke. Meneja wa RUWASA na Ofisa Mazingira shirikianeni na viongozi wa kata, kesho (jana) nendeni mkamtoe bali mbakize mizinga yake ya nyuki tu, na muweke mipaka ya vyanzo vya maji,"amesema Lazaro.
Pia, amewataka watumishi wa Serikali ngazi ya kata na vijiji wakae na kuishi kwenye maeneo yao ya kazi, kwani kwa muda mfupi amebaini wanaozorotesha utendaji kazi za Serikali ni watumishi wanaoishi nje ya maeneo yao ya kazi.
Lazaro ametaka Shule ya Msingi Mkuzi ifanyiwe ukarabati ikiwa ni pamoja na darasa la watoto wenye mahitaji maalumu. Pia ametaka kuvunja moja ya vyoo vya shule hiyo kwani ni tishio kwa usalama wa wanafunzi.
Shekilindi alisema katika Kata ya Migambo ni Kijiji cha Milungui ndiyo kilikuwa hakina umeme, lakini sasa umeme unakwenda huko. Barabara ya lami (Lushoto- Mlola kilomita 44) imefika Migambo, na mipango yao kwa sasa ni kuomba kila mwaka ijengwe kwa kilomita tatu badala ya moja.
"Inashangaza kuna barabara hazijaingia kwenye bajeti ya TARURA kama ile kutoka Migambo kwenda Shule ya Sekondari ya Wasichana Kifungilo. Hii ni shule ya kitaifa na kimataifa, lakini TARURA haijatenga fungu lolote kwenye bajeti yao,"amesema Shekilindi.
Shekilindi aliwahakikishia wananchi hao kupata maji ikiwemo kuongeza mabomba makubwa ili mradi wa zamani uendelee kutoa maji, lakini kuna mradi mkubwa wa maji wa kata 13 huo utaondoa kabisa tatizo la maji Jimbo la Lushoto ikiwemo Kata ya Migambo.
Awali, Diwani wa Kata ya Migambo, Ramadhan Kaoneka alisema kuna wananchi wanachafua vyanzo vya maji kwenye Kitongoji cha Kwaboli kilichopo Kijiji cha Migambo, hivyo kuhatarisha wananchi kukosa maji ya uhakika.