Na Hadija Bagasha, Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashimu Mgandilwa amewataka madiwani wa Halmshauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Mgandilwa ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani cha kupitia taarifa za hesabu za mwisho kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Amesema, fedha nyingi za miradi ya maendeleo zinaweza kutumiwa vibaya ikiwa madiwani watashindwa kutekeleza wajibu wao wa kuangalia thamani ya kiwango cha fedha kinachotumika.
DC Mgandilwa amesema, ni wajibu wa madiwani kuhakikisha wanasimia ipasavyo matumizi ya fedha zinazotolewa kwenye miradi inayotekelezwa kwa kuhakikisha wanasimamia kiwango cha fedha kilichotolewa na kazi husika iliyofanyika.

"Ni jukumu letu sisi madiwani tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa na madiwani wengine katika maeneo mengine juu ya matumizi yetu katika makusanyo na hata matumizi ya fedha za miradi niwaase madiwani wenzangu tuchape kazi tuzitumie kwa malengo yaliyokusudiwa fedha zinazotolewa kwajili ya wananchi wetu, "alisisitiza Naibu Meya Colvas.
Katika kikao hicho Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja Mstaafu Hamisi Mkoba amewataka madiwani wa jiji la Tanga kujitafakari na kuhakikisha katika vikao vyao wanajadili vitu vyenye tija kwa wanachi wao.

Aidha Mwenyekiti Mkoba amewataka madiwani hao kuhakikisha wanapitia kwa kina taarifa hiyo ya fedha waliyofikishiwa ili kuweza kuhoji pale watakapoona panahitaji kufanyiwa marekebisho.
"Niwaambie tu kuwa Mheshimiwa Rais amekuwa anapigia makelele na kusisitiza maamuzi katika vikao sasa kama tunakuja tunakaa dakika tano...dakika mbili tunasema tumemaliza inakuwa, hakuna litakalofanyika,"amesema Meja Mstaafu Mkoba.