NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, nchi inakwenda vizuri ikiwemo kutatua changamoto za sekta mbalimbali ikiwemo afya.
Pia amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kutambua umuhimu wa kuongeza wigo wa huduma za dharura katika maeneo mbalimbali nchini. Dkt.Kikwete amesema, Rais Samia analeta matumaini kwa Watanzania kwa manufaa ya nchi ya leo na kesho.
Mheshimiwa Dkt.Kikwete ameyasema hayo wakati wa kutembelea eneo litakalojengwa mradi wa jengo la matibabu ya dharura katika katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze iliyopo Msoga mkoani Pwani chini ya ufadhili wa Kampuni ya ABBOTT Fund ya nchini Marekani kwa gharama ya sh.Bilioni 1.2.
Pia amesema, ABBOTT wameanza kusaidia na kushirikiana na Serikali ya Tanzania tangu mwaka 2002 ambapo walianza na ugonjwa wa Ukimwi, ujenzi wa maabara na sasa miradi ya majengo ya dharura.
Dkt.Kikwete amesema kuwa,msaada uliotolewa kwa ajili ya jengo hilo ni sh.bilioni 1.2 ikiwa ni sawa na dola 500,004 na tayari walishashiriki kusaidia masuala mbalimbali nchini ikiwemo kutoa vipimia VVU vipatavyo millioni moja.
“Sijafanikisha peke yangu hili,mie niliweka msukumo,lakini namshukuru sana Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati huo, Dorothy Gwajima ambaye ndie 'alipush' (alisukuma) suala hili. Niseme tu, namshukuru sana,”amesema Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.
Pia Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Kikwete ameiomba Serikali itoe mafunzo kwa madaktari na watumishi wa afya kuhusiana na masuala ya dharura ili miradi kama hiyo itakapokamilika kusiwepo na changamoto ya ukosefu wa wataalamu wa dharura.
Ameiomba jamii na watumishi wa umma waendelee kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchapa kazi na kuwataka vijana kujituma ili kujiepusha na kuwa mzigo katika jamii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto,Dkt.Godwin Molell amesema, Serikali imetenga sh.bilioni 187 kwa ajili ya kujenga kiwanda cha chanjo za UVIKO-19 ambazo zitazalishwa nchini.
Dkt.Mollel amesema, Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kununua magari ya wagonjwa 150 ambayo yatasambazwa nchini ambapo kati ya hayo Jimbo la Chalinze litapatiwa gari moja kati ya hayo.
Amesema, Mbunge wa Jimbo la Chalinze,Ridhiwani Kikwete aliomba sh.milioni 418 na Serikali imeridhia kutoa fedha hizo kwa awamu kwa ajili ya umaliziaji wa majengo ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.
Wakati huo huo,Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete amesema juhudi zinaendelea kumaliza baadhi ya majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze, ambayo imetolewa shilingi bilioni moja katika ujenzi wa majengo matano ambayo yamefikia asilimia 83 kukamilika.
Naye Mwakilishi wa ABBOTT,Frenk Kanza amesema, kampuni hiyo inajishughulisha kutengeneza bidhaa za maabara Duniani ila kwa msaada huu umetokana na fedha kutoka mfuko wa uwezeshaji wa masuala ya afya. Kanza ameishukuru Serikali kwa msamaha wa kodi dola 40,000.
Amesema,mradi huu utaleta mapinduzi makubwa katika masuala ya kiafya katika wilaya ya Chalinze na Mkoa wa Pwani kwa ujumla.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallah ameeleza kuwa, halmashauri imepata mradi mkubwa wa ujenzi wa jengo la dharura kupitia ufadhili wa ABBOTT.
“Mradi huu unaokwenda kujengwa kwenye Hospital ya Wilaya ya Msoga ni matokeo makubwa ya maombi toka kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne ,mzee Jakaya Mrisho Kikwete kwenda kwa Rais wa ABBOT,"amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa, mkoa una maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji hivyo itapendeza kiwanda cha chanjo ya UVIKO-19 kikajengwa mkoani Pwani.