Na Robert Kalokola,Geita
Uongozi wa Shule ya Emaco Vision iliyopo Kata ya Nyankumbu,Halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita umeiomba jamii,wazazi ,wamilki wa shule na wanafunzi kuunga mkono juhudi za Waziri wa Elimu na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kudhibiti na kukemea vitendo vya kinyume na maadili vya kufanya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa .
Mwalimu mkuu wa shule ya Emaco Vision, Octavian Laurian akizungumzia wizi wa mitihani ( Picha na Robert Kalokola).
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Oktavian Laurian amesema vitendo vya udanganyifu katika mitihani hasa ya kitaifa haiwezi kufanywa na wanafunzi na walimu tu bila Menejimenti za shule kuhusika hivyo ameshauri nguvu kubwa ielekezwe kwenye kuandaa wanafunzi darasani kuliko kujihusisha na wizi wa mitihani.
Amesema kuwa, shule hiyo imeandaa wanafunzi wake vizuri kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la saba na wamekuwa wanafanya vizuri kwenye mitihani ya ndani ya upimaji kama vile mkoa na wilaya,hivyo aanaamini kwenye mtihani wa taifa wa darasa la saba unaoanza kufanyika Septemba 8,mwaka huu wanafunzi wa shule hiyo watafaulu vizuri.
Mwalimu Oktavian Laurian amesema kuwa shule hiyo ina jumla ya watahiniwa 88 ambao wanategemewa kufanya mtihani wa darasa la Saba na watahiniwa 43 wavulana na wasichana ni 45 na kusisitiza kuwa shule hiyo haivumilii aina yoyote ya udanganyifu katika mitihani.
Grace Maganga Mtahiniwa wa darasa la saba katika shule ya msingi Emaco Vision Mjini Geita ( Picha na Robert Kalokola).
Wanafunzi waliozungumza na Diramakini Blog wameonyesha kujiamini katika masomo yao wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mitihani yao kwa sababu ya kumaliza mada zao zote za masomo na kufanya mitihani mingi ya majaribio ya mara kwa mara.
Jesca Salim (13) Mwanafunzi wa darasa la Saba amesema ana ndoto ya kuwa rubani wa kuendesha ndege hivyo amesema kwa namna walivyo fundishwa kwa bidii na walimu wao anaamini maswali ya mitihani yatatokana na yale waliyosoma darasani hivyo atafaulu na kufikia malengo yake.
Amewataka baadhi ya wadau wa elimu wanaojihusisha na wizi wa mitihani kuacha kwani kufanya hivyo ni kukatisha ndoto za wanafunzi hao inapotokea imebainika na kufutiwa mitihani hivyo kukosa mwelekeo.
Elia Simon Mtahiniwa darasa la 7 shule ya msingi Emaco Vision mjini Geita (picha na Robert Kalokola).
Naye Mwanafunzi Grace Maganga (13)amesema wanafunzi wasishirikishwe kwenye udanganyifu wa mitihani badala yake yasikilize walimu wao darasani na kusoma kwa bidii kwani wakisoma na kumaliza mada zote hawawezi kushindwa mitahani na malengo yao yatatimia.
Ameeleza kuwa yeye ana ndoto ya kuwa Daktari wa Macho na kutokana na maandalizi aliyo yafanya kwa kusoma kwa bidii anaamini katika mtihani wake wa kumaliza darasa la saba atafaulu vizuri na kuanza kidato cha kwanza kwa ufaulu wa daraja la kwanza.
Joseph Enock ambaye ni mmoja wa wazazi wa wanafunzi waliofika katika shule hiyo ili kufanya maombi maalum kwa ajili ya kuombea watoto wao ili waweze kufanya vizuri kwenye mitiha ya yao ya darasa la saba amesema tabia za kuiba mitihani ni mbaya na inatia hasara kwa taifa na mzazi mmoja mmoja.
Akram Byarushengo mtahiniwa darasa la saba shule ya msingi Emaco Vision mjini Geita (Picha Robert Kalokola).
Amesema kuwa, watoto wanaoiba mitihani wanakuwa hawana uwezo unaotakiwa ili kumudu masomo ya ngazi ya juu wanayo chaguliwa kuingia hivyo kuwafanya wachukie masomo na kuacha shule kwa kukata tamaa.
Lakini pia amesema wazazi wanapoteza raslimali fedha nyingi ambazo wanatumia kulipia watoto wao na baadae kushindwa kuendelea na masomo kwa kuchaguliwa kuendelea na masomo ya ngazi ya juu yake kutokana na matokeo ya kuiba mtihani.
Amewaomba wadau mbalimbali katika sekta ya elimu kujiepusha na udanganyifu wa mitihani bali waelekeze nguvu kubwa kuwapeleka katika shule zinazo fundisha vizuri ili wanafunzi waweze kufaulu kwa juhudi zao binafsi.
Liston John mtahiniwa wa mtihani wa darasa la Saba shule ya msingi Emaco Vision mjini Geita (Picha na Robert Kalokola)
Akitoa taarifa kwa umma kuhusu kufanyika kwa mitihani hiyo ya darasa la Saba Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani nchini Daktari Charles Msonde amesema kuwa watahiniwa wote wanaoterajiwa kufanya mtihani ni 1,132,143 ambapo wasichana 584,641 sawa asilimia 51.6 wavulana 547502 sawa na asilimia 48.36.
Shule ya Msingi Emaco Vision imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa kushika nafasi kati ya 100 na 200 kitaifa huku kimkoa na wilaya ikishika nafasi kati ya 1 na 3 katika mitihani ya kitaifa na mitihani ya ndani ya upimaji.