Na Hadija Bagasha, Tanga
Serikali imeshauriwa kuja na mpango mkakati wa kuliweka suala la dawa za kulevya kwenye mtaala wa kielimu kuanzia ngazi ya msingi kutokana na stadi zilizofanyika kubaini kuwa kuna tatizo kubwa kwenye shule za msingi, kwa kuwa watoto wanaanza kutumia dawa hizo mpaka wanapofikia sekondari au vyuo wanakuwa tayari wameshakuwa waathirika wakubwa wa tatizo hilo.
Ushauri huo umetolewa na Irene Kaoneka ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya CASA FAMILIA ROSSETA inayojihusisha na kulea watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalumu wakati wa kampeni ya kupambana na dawa za kulevya kwa kushirikisha midahalo mbalimbali kwenye shule zaidi ya 38 jijini Tanga ikiwemo shule ya Sekondari Galanosi.
Mkurugenzi Irene amesema, ipo haja ya serikali kuja na mpango huo ili kunusuru vizazi vijavyo na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya kwani watajapokutana na somo hilo kuanzia ngazi ya shule ya msingi itasaidia wao kujitambua na kujua madhara yake kwa haraka.
Amesema, vijana wengi walio kwenye uraibu wa matumizi ya Dawa za Kulevya walianzia wakiwa kwenye Elimu ya Msingi hivyo ni vyema Serikali ikawaliweka suala hilo kwenye mitaala ya kielimu lengo likiwa kuwafundisha elimu ya kujitambua mapema.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwanyanyapaa watumiaji wa dawa za kulevya na badala yake amewataka wawasaidie kuwapeleka katika vituo vitakavyowasaidia kupata utabibu.
Kwa upande Daktari katika fani ya afya ya akili kutoka hospitali ya rufaa ya Mkoa Tanga Bombo, Dokta Wallace Karata amesema kuwa, katika kampeni wanazofanya wamelenga shule za sekondari kwakuwa ndio wanafunzi wanaoweza kujipambanua ili kuwalinda watoto wa shule za msingi.
"Tumelenga zaidi Shule hasa ngazi ya Sekondari kwakuwa hawa ndio wanaonekana kuwa kwenye hatari zaidi kuliko makundi mengi na tutazunguka kuwapatia Elimu hii hivyo niwaombe vijana waachane na tabia hii ya matumizi ya dawa za kulevya," alisema Karata.
Dkt.Karata amesema kuwa, Mkoa wa Tanga ni mkoa wa pili kwa matumizi ya dawa za kulevya hivyo ipo haja ya kuendelea na mapambano dhidi ya dawa hizo wakiamini elimu na midahalo ambayo wamekuwa wakiifanya itakuwa njia bora ya kuisadia jamii hivyo wameomba kuungwa mkono.
Baadhi ya wanafunzi akiwemo Iddy Jumanne na Innocent Patric wameiomba serikali kuanzisha sera sahihi katika upambanaji wa dawa za kulevya kwa kuwa hivi sasa watumiaji wa dawa hizo hawajifichi huku mwalimu Leonard Ojoi wa shule ya Galanosi Sekondari akisisitiza wazazi na walimu kufuatilia mienendo ya watoto wao.
Zaidi ya shule 38 za jiji la Tanga zimeweza kufikiwa katika kampeni ya kutoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya lengo likiwa ni kuwalinda watoto wadogo wa shule za msingi ambao hawawezi kujipambanua.