Na Tito Mselem
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, leo Septemba 14, 2021 amezindua rasmi Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizindua rasmi Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, leo Septemba 14, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia amesema lengo la Mkakati huo ni kupata taarifa sahihi za idadi ya watu waliopo nchini ikiwemo jinsia, elimu, afya na hali za ajira ili kuwa na takwimu sahihi zitakazoiwezesha Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya watu wake.
“Taarifa za Sensa zitatusaidia kujua idadi ya watu wapi walipo, elimu zao, afya zao, hali ya ajira zao pamoja na makazi yao, pia zitatusaidia kujua ongezeko la watu wetu ili tuandae Sera ya Taifa na kujua mgawanyo wa rasilimali kwa uwiano sawa kwa wananchi wetu,” amesisitiza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema, haiwezekani kupeleka huduma kwa wananchi wa eneo fulani kama haijulikani idadi ya watu katika eneo husika ambapo amewataka wananchi wote wakaolala ndani ya mipaka ya Tanzania usiku wa kuamkia siku ya sensa kushiriki zoezi hilo.
Pia, Rais Samia amesema, Taarifa za sensa hutumika pia kwa watafiti wengi wa ndani na nje ya nchi katika shughuli zao mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo ya kijami, kisiasa na kiuchumi.
Kufuatia hatua hiyo, Rais Samia ametoa wito kwa viongozi mbalimbali nchini wakiwemo viongozi wa dini, kuhakikisha wanawahamasisha wananchi ili washiriki kikamilifu katika zoezi la sensa litakalofanyika Agosti 2022.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema jukumu la kusimamia zoezi la sensa lipo chini ya ofisi yake pamoja na ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambapo amemuhakikishia Rais Samia kwamba watu wote watakaolala ndani ya mipaka ya Tanzania kuamkia siku ya sense watahesabiwa.
“Sina Shaka na nikuhakikishie Mhe. Rais kwamba, maagizo yako yote uliyoyatoa tutayafanya kama ulivyoelekeza na nikuahidi kwamba watu wote watakaolala ndani ya mipaka ya Tanzania kuamkia siku ya sensa watahesabiwa,” amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko, amewataka wadau wote wa madini nchini kuhakikisha wanashiki kikamirifu katika zoezi la kuelimisha na kuhamasisha wananchi juu ya Mkakati wa sensa uliyozinduliwa na Rais Samia jijini Dodoma.
“Naomba nichukue fursa hii kuwataka wadau wote wa madini hususan viongozi katika migodi yote nchini na maeneo yenye shughuli za madini kuhakikisha wanashiriki katika uhamasishaji na uelimshaji juu ya umuhimu wa sensa katika kupanga mipango ya kitaifa,” amesema Waziri Biteko.
Sensa inayotegemea kufanyika 2022 chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani ni Sensa ya Sita tokea nchi hiyo imepata uhuru wake mwaka 1961 iliyobebwa na kaulimbiu ya “Sensa kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa”.
Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia) akifuatilia uzinduzi wa Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, leo Septemba 14, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo kwenye uzinduzi wa Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, leo Septemba 14, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.