Na James K. Mwanamyoto, Dodoma
Serikali imetoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa lengo la kuwawezesha wajumbe hao kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na ulinzi wa rasilimali za umma.

Akizungumza katika semina hiyo Septemba 7, 2021, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, Waheshimiwa wajumbe wa kamati hiyo watapata fursa ya kufahamu vema makosa ya rushwa kama yanavyotamkwa katika Sheria Na. 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007 na hatimaye kuwa na mchango mkubwa wa kutetea mapendekezo ya maboresho ya sheria hiyo pindi itakapowasilishwa Bungeni.
“Ikumbukwe kuwa, tunayo sheria ya muda mrefu ya kuzuia na kupambana na rushwa inayohitaji maboresho hivyo, naamini wajumbe wa kamati hii kupitia elimu mtakayoipata mtatoa mchango mkubwa wa kuiboresha,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Ameongeza kuwa, ni wakati muafaka kwa wajumbe wa kamati hiyo kuielewa vema Sheria hiyo Na. 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007 na kuwa mabalozi wazuri kuhimiza maboresho yake ili iwe na manufaa katika mapambano dhidi ya rushwa na ulinzi wa rasilimali za umma kwa ujumla.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo (Mb) amesema kamati yake imehudhuria mafunzo hayo yenye lengo la kuwaelimisha namna ya kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa ili nao waweze kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa nchini.






Aidha, Mhe. Chaurembo ameongeza kuwa, Serikali inapeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwenye halmashauri, hivyo amemuomba Mhe. Mchengerwa kuhakikisha TAKUKURU inaendelea kutoa mafunzo ya mapambano dhidi ya rushwa katika halmashauri zote kwa lengo la kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma zinazotolewa na Serikali ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Naomba halmashauri zote nchini zipatiwe mafunzo ya kupambana na vitendo vya rushwa wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuwezesha fedha za walipa kodi wa kitanzania kutumika vizuri,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema, semina hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imelenga kubadilishana uzoefu, kutoa elimu ya kupambana na rushwa na kutekeleza takwa la kisheria ambalo linaitaka TAKUKURU kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.