Katibu Mkuu TUGHE aiangukia Kamati ya Wanawake kuhusu Rais Samia

Na Rotary Haule, Dodoma

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Hery Mkunda ameiangukia Kamati ya Wanawake ya chama hicho kuhakikisha wanamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kufanya kazi kwa urahisi zaidi.
Mkunda ametoa ombi hilo leo wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa wanawake wa chama hicho unaofanyika katika Ukumbi wa ST Gaspar jijini Dodoma.

Amesema, wanawake wana nguvu kubwa ya kuleta ushawishi sehemu yoyote, lakini ni vizuri wakatumia nguvu hiyo kuleta ushawishi katika kumsaidia Rais Samia kufanya kazi zake kwa wepesi zaidi.

"Wanawake wana nguvu na ushawishi mkubwa, kwa hiyo niwaombe msiwe kikwazo kwa mama Samia, bali mpeni nguvu kubwa ya kufanya kazi ili aweze kufikia malengo ya kuijenga nchi yetu,"amesema Mkunda.

Aidha, Mkunda amesema wanawake ni tegemeo kubwa na wamekuwa na uwezo mkubwa katika kusimamia shughuli mbalimbali huku akitolea mfano kuwa taasisi yoyote ikiongozwa na mwanamke inafanya vizuri kuliko ikisimamiwa na mwanaume.

Mkunda ameongeza kuwa, TUGHE inawategemea sana wanawake na hata mafanikio yaliyopatikana katika chama hicho yametokana na nguvu ya wanawake huku akisema TUGHE haiwezi kusimama bila ya kuwepo kwa wanawake.

"Taasisi nyingi ambazo mtendaji wake mkuu anakuwa mwanamke zinafanya vizuri sana kuliko zile zinazosimamiwa na wanaume ndio maana TUGHE inawapa nafasi kubwa wanawake ili kuhakikisha chama kinaendelea kusimama kikamilifu," ameongeza Mkunda.

Hata hivyo,amewaomba wajumbe wa mkutano mkuu wa wanawake hao kuhakikisha wanasimama imara katika kuchagua viongozi wazuri na makini ambao watakivusha chama kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Archie Ntambo amesema, wanapochagua viongozi lazima wawe makini na kamwe wasichague viongozi kwa kufuata pesa,uchawi na hata ulaghai.

Ntambo amesema kuwa, wanachama wa TUGHE hasa wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa mahali pa kazi na hivyo ili kupata majibu ya changamoto hizo lazima wachague viongozi makini na wenye msaada kwao.

Naye Mwenyekiti wa Wanawake Taifa, Jane Madete amesema wanawake lazima wafanye maamuzi sahihi ili TUGHE iendelee kuwa imara huku akishukuru chama hicho kwa kubeba hoja zao kiasi ambacho kimepelekea kamati za wanawake kutambulika kikatiba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news