Na Robert Kalokola, Diramakini Blog
Serikali imeahidi kufanya mabadiliko ya kisera,kisheria na kikanuni katika sekta ya madini nchini ili kuwezesha wachimbaji wadogo kufanya kazi zao kwa ufanisi ili kuwawezesha kuchangia katika uchumi wa taifa na kunufaika na mapato yatokanayo na madini.
Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza katika Maonesho ya Nne ya Uwekezaji na Teknolojia katika Sekta ya Madini mjini Geita alipomwakilisha Makamu wa Rais kuyafunga rasmi. (Picha na Robert Kalokola).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt.Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philipo Mpango wakati akifunga rasmi maonesho ya nne ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini mjini Geita leo Septemba 26,mwaka huu.
Amesema kuwa, malengo ya Serikali ni kuondoa changamoto zote zinazowakwaza wachimbaji wadogo ili kutengeneza mnyororo wa thamani katika kuchangia uchumi wao na kuinua uchumi wa nchi na Watanzania kwa ujumla.
Amesema kuwa, ili kuweza kufanya madini yachangie uchumi wa nchi ni kusimamia kanuni za kushirikisha wazalendo katika kutoa huduma na bidhaa ( local content) na kuongeza thamani ya madini hapa hapa nchini kwa kujenga viwanda vya kuasafisha madini ili kuyaongezea thamani na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwigulu Nchemba akizungumza na mjasiriamali katika banda lake kwenye maonesho ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Amefafanua kuwa, ujenzi wa viwanda vya kusafisha dhahabu kama kile cha Geita na Mwanza pamoja na kiwanda cha kusafisha madini ya Shaba kinachojengwa Bagamoyo mkoani Pwani vitasaidia kuimarisha uchumi.
Waziri Nchemba amewataka wachimbaji wadogo kujenga tabia ya kusaidiana katika kazi zao za uchimbaji kwa kutooneana wivu badala yake wafanye kazi pamoja ili waweze kuboresha maisha yao bila kuwa na migogoro.
Amepongeza jitihada za Wizara ya Madini kupunguza matatizo ya wachimbaji wadogo, kugundua maeneo yenye madini ya dhahabu lakini baada ya kutoa taarifa na kutaka wapewe leseni, wanajikuta wamepewa watu wengine ambao ni tofauti na wao waliogundua.
Naibu Waziri wa Madini Profesa Shukrani Manya. (Picha na Robert Kalokola)
Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya anasema kuwa usimamizi wa kanuni za makampuni makubwa kushirikisha wazawa au wazalendo katika shughuli zao za huduma na bidhaa (local content) imechangia kwa kiwango kikubwa kuboresha maisha ya wananchi ambao wanaishi maeneo yanapochimbwa madini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akungumza katika kufunga maonesho ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema kuwa, maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Mkoa wa Geita na taifa kwa ujumla na yamekutanisha taasisi ya umma na binafsi pamoja na wachimbaji wadogo walioshiriki maonesho hayo zaidi ya 500.
Amesema kuwa, maonesho hayo ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini yametangazwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa ya kitaifa kuanzia mwakani, hivyo mkoa umeanza kubuni miradi ya kimkakati katika eneo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amemuomba Waziri wa Madini kupokea maombi ya mkoa ya kusaidiwa kupata fedha za kujenga miradi ya mkakati ya Halmashauri ya Mji wa Geita katika eneo hilo la maonesho la EPZA.
Makamu wa Rais wa Mgodi wa kuchimba Dhahabu wa Geita (GGML), Simon Shayo amesema kuwa, katika kufanya malengo ya serikali ya kutaka sekta ya madini ichangie pato ghafi taifa kwa asilimia kumi mgodi huo unatamani mchango huo ufike asilimia ishirini na tano.
Shayo ameongeza kuwa, katika kusaidia jamii na kufungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine, mgodi huo kwa mwaka huu umefanya biashara na wazabui wa Geita 360 yenye thamani ya dola milioni 10.
Aidha, amesema kuwa GGML imefanya biashara kupitia wazabuni wa ndani kwa kutoa huduma pamoja na huduma zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 60 ambazo zitasaidia katika kuchangia katika uchumi wa nchi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo mkoa wa Geita (Gerema) Christopher Kadeo ameomba Serikali kusaidia wachimbaji wadogo kuchoronga miamba kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Baadhi ya wananchi wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba katika kufunga maonesho ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Aidha, ameomba taasisi hiyo kuwezesha wachimbaji wadogo katika mkoa huo kuwa na migodi ya kudumu ili waweze kuchimba kwa muda mrefu na kwa tija na kushindana na makampuni mengine makubwa.
Kadeo ameiomba Serikali kusaidia wachimbaji wadogo wa madini kuongeza msukumo ili taasisi ,za kifedha ziweze kutoa mikopo kwao ili kuweza kumudu kununua vifaa vya kuchimbia na shughuli nyingine za uchimbaji wa madini.
Maonesho ya uwekezaji na teknolojia katika sekta ya madini yalianza rasmi Septemba 16, mwaka kwa kuzinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Septemba 22, mwaka na kufungwa rasmi leo Septemba 26, Mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba.