Mashine ya kuangalia mapigo ya moyo, upumuaji yaibiwa hospitali

Na Derick Milton, Simiyu

KATIKA hali asiyokuwa ya kawaida mashine inayotumika kuangalia maendeleo ya mgonjwa wakati wa upasuaji ikiwemo mapigo ya moyo, wingi wa hewa ya Oksijeni kwenye damu pamoja na upumuaji imeibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.

Kifaa hicho kinadaiwa kuibwa usiku wa kuamkia siku ya Jumapili Septemba 20/09/2021 wiki iliyopita, kikiwa katika chumba cha upasuaji mkubwa namba mbili katika hospitali hiyo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt.Mike Mabimbi alisema kuwa, upotevu wa kifaa hicho uligundulika baada ya mmoja wa madaktari siku ya Jumatatu asubihi kuhitaji kutumia mashine hiyo.

Alisema kuwa, daktari huyo (hakumtaja jina) mara baada ya kufika katika chumba hicho kwa ajili ya kutaka kumpima mgonjwa, ndipo aligundua kutokuwepo kwa mashine hiyo.

“Mashine yenyewe ndiyo ambayo imechukuliwa, huku stendi yake ikiwa imeachwa, pamoja na vifaa vingine, mazingira yanaonyesha kuwa mashine hii iliibiwa usiku wa kuamkia siku ya Jumapili wiki iliyopita,” amesema Mabimbi.

Aidha, mganga mfawidhi huyo amesema kuwa siku ya Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi wakati wanafanya ukaguzi kwenye vyumba vyote vitatu vya upasuaji, mashine hiyo ilikuwepo.

Amesema kuwa, watumishi sita ambao wamekuwa wakifanya kazi kwenye chumba hicho, wakiwemo madaktari watatu na wauguzi watatu wamehojiwa na uongozi wa hospitali hiyo kujua mazingira ya upoteaji wa kifaa hicho.

“Kati ya watumishi wote sita, mmoja amegoma kuhojiwa, wengine wote wamekana kuhusika na wizi huo na wanadai kuwa kifaa hicho walikiacha mara baada ya kazi,” amesema Mabimbi.

Aidha, amesema kuwa kutokana na hali hiyo wametoa taarifa jeshi la polisi na kufungua kesi BRD/RB/2342/2021 ikiwa pamoja na kutoa taarifa Wizara ya Afya kwa ajili ya hatua nyingine zaidi.

Dkt.Mabimbi amewataka watu ambao wamehusika na wizi wa kifaa hicho, kukirejesha mara moja kwani serikali ilikileta kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news