Masomo ya Sayansi na Teknolojia yanalipa, tuwekeze nguvu huko-January Kirambata

Na Yusuph Mussa, Korogwe

BAADHI ya wadau wameshauri masomo ya sayansi na teknolojia yawekewe mkazo kuanzia elimu ya msingi, kwani kutokana na mabadiliko ya Dunia kutawaliwa na Sayansi na Teknolojia, kutawezesha wanafunzi kukabiliana na soko la ushindani duniani.
Wahitimu wa darasa la awali Shule ya Mchepuo wa Kingereza ya Hills View iliyopo Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, wakiingia jukwaani ili kuimba wimbo. Ni kwenye mahafali ya 23 ya darasa hilo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Ukumbi wa Taasisi ya Rock Memorial Education Trust (RMET) mjini Korogwe, ambayo ndiyo inamiliki shule hiyo.

Hayo yalisemwa Septemba 4, 2021 na Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Korogwe January Kirambata kwenye mahafali ya 23 ya darasa la awali na ya 16 ya darasa la saba katika Shule ya Mchepuo wa Kingereza ya Hills View iliyopo Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga.

Kirambata alisema, pamoja na masomo hayo ya sayansi, lakini ili kufikia soko la ajira duniani na kukabiliana na utandawazi, lugha ya Kiingereza bado ni muhimu kufundishia shuleni, hivyo ipo haja ya kuwaandaa wanafunzi katika mapambano ya utandawazi.

"Mtakubali kuwa vijana hawa wamelelewa katika msingi mzuri. Wanaonekana nadhifu, wenye nidhamu na furaha, kwani wapo kwenye mazingira rafiki ya kujifunzia. Na hii ndiyo siri ya mafanikio, na ndiyo maana shule hii imekuwa king'ang'anizi katika nafasi za juu kiwilaya na kimkoa. Na hii inatokana na kujiwekea malengo mazuri.
Wahitimu wa darasa la awali Shule ya Mchepuo wa Kingereza ya Hills View iliyopo Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, wakiingia jukwaani ili kuimba wimbo. Ni kwenye mahafali ya 23 ya darasa hilo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Ukumbi wa Taasisi ya Rock Memorial Education Trust (RMET) mjini Korogwe, ambayo ndiyo inamiliki shule hiyo.

"Wanafunzi mnaobaki nawaasa kufuata nyayo za wahitimu hawa. Kuweni wavumilivu, kwani mvumilivu hula mbivu. Hakuna njia ya mkato katika maisha. Someni kwa bidii mkizingatia kuwa Serikali ya Tanzania inakazania masomo ya sayansi, kwani sayansi na teknolojia imeifanya dunia imekuwa kijiji, hivyo kama hukusoma masomo hayo, unaweza kuwa nje ya utandawazi ikiwemo ajira, uchumi na biashara," alisema Kirambata.

Alisema kwa wahitimu kukaa hapo wengine tangu madarasa ya awali huku wengine wakianzia darasa la kwanza, ana uhakika wameiva kujiunga na masomo ya sekondari, kwani masomo yote hapo shuleni (kasoro kiswahili), wamejifunza kwa lugha ya kingereza, ambapo lugha hiyo bado ni msingi kwa masomo ya sekondari, kwani masomo yote huko yanafundishwa kwa kingereza kasoro Kiswahili tu.

Kirambata aliipongeza Taasisi ya Rock Memorial Education Trust (RMET) chini ya Mkurugenzi Mtendaji Sylvester Mgoma ambayo ina shule ya awali, msingi, sekondari na chuo cha ualimu, kwani imekuwa ikiwalea watoto wadogo kwa kuwapa elimu ya awali ambao ndiyo msingi wa elimu kwa mtoto.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Hills View Charles Mhuza alisema wahitimu wa darasa la awali ni 50 ambapo wasichana ni 23 na wavulana 27. Na wahitimu wa darasa la saba ni 43, ambapo wavulana ni 17 na wasichana ni 26, na kujinasibu kuwa wanafunzi hao wanaojiandaa na mtihani wa Taifa wa darasa la saba Septemba 8 na 9, 2021 watafanya vizuri.
Wahitimu wa darasa la saba Shule ya Mchepuo wa Kingereza ya Hills View (kushoto) iliyopo Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, wakiingia ukumbini. Ni kwenye mahafali ya 16 ya shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Ukumbi wa Taasisi ya Rock Memorial Education Trust (RMET) mjini Korogwe, ambayo ndiyo inamiliki shule hiyo. Waliotangulia mbele ni Wahitimu wa Darasa la Awali wa Shule hiyo ambao kwao ni mahafali ya 23.

"Shule yetu ya msingi ya Hills View imekuwa ikifanya vizuri, mara zote imekuwa ikishika nafasi ya kwanza au ya pili kiwilaya mara moja moja kiwilaya, na mwaka jana (2020) imechukua nafasi ya 18 katika mkoa mzima wa Tanga ambao ulikuwa na shule 476 zenye wanafunzi chini ya 40.

"Pamoja na mafanikio hayo, wanafunzi wetu pia wamekuwa wakifanya vizuri huko waliko kwenda kuendelea na masomo na kufanya vizuri kidato cha nne baadae kidato cha tano na sita, na kuendelea vyuo vikuu, na kutoa wataalamu wakiwemo wahandisi, marubani, madaktari, wanasheria na kada nyingine," alisema Mhuza.

Mhuza alisema pamoja na kutoa elimu ya darasani, bado wamekuwa na ziara ya mafunzo kwenye taasisi za Serikali na binafsi, ambapo Agosti 27 hadi 29, mwaka huu, wanafunzi wote hao wa darasa la saba wanaohitimu walikwenda jijini Tanga na kutembelea Kiwanda cha Maziwa cha Tanga Fresh, Bandari, Soko la Tangamano, Kanisa Kuu Katoliki la St. Anthony, Chumbageni, Mapango ya Amboni na kwenda Ufukwe wa Bahari ya Hindi kuogelea.

Mkurugenzi wa Taasisi ya RMET, Mgoma aliwataka wahitimu hao kupambana kuona wanaendelea kufanya vizuri kwa kuitangaza shule hiyo, kwani karne ya 21 ni ya ushindani kwenye elimu, huku akiamini wanafunzi hao wameiva kukabiliana na ushindani mbele yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news