NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Mheshimiwa Hassan Mtenga Agosti 29, 2021 amezindua mradi wa uchimbaji wa visima vya maji 30 katika Kata ya Magomeni Mtaa wa Magomeni Kagera ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwa kumtua mama ndoo kichwani.
Mradi huo ambao unasimamiwa na Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini utagharimu kiasi cha shilingi milioni 980 hadi kukamilika kwake na utatekelezwa katika vijiji 30 vilivyopo katika majimbo 10 ya Mkoa wa Mtwara, ambapo kila jimbo litapata visima vitatu.
Ili mradi huo uwe endelevu, Mheshimiwa Mtenga amewataka wananchi wa Mtaa wa Kagera kuhakikisha wanaimarisha ulinzi wa mradi huu kuanzia sasa hadi pale utakapokamilika.
"Visima tunavyovijenga vinahitaji ulinzi wa hali ya juu, mmesikia wenyewe gharama yake ni kubwa mno uangalifu unahitajika sana,"amesema Mheshimiwa Mtenga.
Pamoja na hilo, Mheshimiwa Mtenga amewataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kujitolea hasa katika Sekta ya Elimu ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta hiyo na kuleta mandeleo.
Naye Mkurugenzi wa Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini, Bw. Jumanne Mpemba ameishurukuru Serikali kwa kuwekeza fedha katika mradi huu ambao utapunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo yaliyoanishwa.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Magomeni Bw. Lameck Mlaponi amemshukuru Mheshimiwa Mtenga kwa kuona changamoto ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Magomeni na kuitolea ufumbuzi.
Naye Asha Shabani mkazi wa Mtaa wa Kagera ameishukuru sana Serikali kwa kuwekeza fedha hizo kwa sababu mradi huo utapunguza changamoto ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.
Kwa Manispaa ya Mtwara-Mikindani visima hivyo vitajengwa katika kata za Mitengo, Magomeni na Ufukoni.