NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma, Jaqueline Msongozi amewataka wanawake nchini kutokubali kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume ambao hawajafanyiwa tohara ili kuondoa hatari ya kupata magonjwa.
Ameyasema hayo leo Septemba 27,2021 wakati Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza ilipotembelea na kukutana na viongozi pamoja na wadau wa mkoa huo.
Pia kamati hiyo imeupongeza mkoa huo kwa mafanikio iliyoyapata katika kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI ambapo mkoa una maambukizi ya asilimia 4.4 chini ya kiwango cha kitaifa cha 4.7.
"Niwashauri wanawake wenzangu wa Rukwa na kote nchini kabla ya kuwa na mahusiano ni vizuri kujua endapo mwanaume amepata tohara au la.Ukikuta hajapata tohara basi usitoe huduma," amesema Mbunge Msongozi.
Mheshimiwa Msongozi amekuwa miongoni mwa wabunge wasiopenda kukaa na jambo moyoni, kwani hivi karibuni alipaza sauti bungeni akilalamikia kitendo cha wabunge wa viti maalumu kunyanyaswa kijinsia, kunyanyapaliwa na kufanyiwa ukatili na vitisho juu na wabunge wa majimbo wanapowajibika kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu Mkoa wa Rukwa, Dkt. Boniface Kasululu, wanaume 34,549 kati ya lengo la watu 35,999 wamepatiwa huduma ya tohara kwenye mkoa huo ikiwa ni mkakati wa kupungunza maambuzi ya VVU/Ukimwi.