Mwenyekiti CCM Mara:Rais Samia Suluhu ametupa heshima Kimataifa

NA MWANDISHI MAALUM

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (No.3) amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa hotuba ya kihistoria katika Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
"Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Septemba 23, 2021 amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa katika uongozi wake, Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na mataifa na wadau wengine duniani kutatua changamoto zinazoikabili Dunia kwa sasa.

"Kwa hakika, ile ni kati ya hotuba bora zaidi kwa Rais wetu katika uso wa Dunia, hii inadhirisha namna ambavyo Mheshimiwa Rais Samia alivyo jasiri na imethibitisha wazi kuwa, anatosha kutuongoza hata baada ya mwaka 2025;

Kiboye ameyasema hayo mjini hapa wakati akizungumzia kuhusiana na hotuba ya Rais Samia wakati akihutubia katika Mkutano wa 76 wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mjini New York, Marekani.

Amesema, miongoni mwa mambo ambayo yalimfurahisha ni pamoja na Rais Samia kutumia hotuba hiyo pia kueleza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi licha ya changamoto za ugonjwa wa UVIKO-19 na kwamba baada ya kushuka kwa ukuaji uchumi kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 5.4 kwa sasa Tanzania inafanya jitihada za kuziinua sekta zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo.

Miongoni mwa sekta hizo ni pamoja na utalii,kuimarisha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji nchini pamoja na kuimarisha misingi ya utawala bora.

"Hatua nyingine nzuri ni pamoja na Mheshimiwa Rais Samia kueleza jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika nyanja za uchumi ikiwa ni pamoja na kuweka sera madhubuti na maboresho ya mfumo wa bajeti ili kupunguza idadi ya wanawake na wasichana wanaoishi katika umaskini. Sisi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara tunaunga mkono juhudi zote za Rais wetu ili aweze kutekeleza mambo haya kwa mafanikio zaidi,"amesema Kiboye.

Katika hatua nyingine, Kiboye ametoa wito kwa watumishi wa Mungu, Watanzania na makundi mbalimbali kuendelea kumuombea Rais Samia na kuunga mkono juhudi zake ambazo zimelenga kuleta neema nchini.

"Tukifanya kazi kwa bidii na kulipa kodi zetu kwa wakati, ikiwemo kuchangia shughuli za maendeleo hiyo pia ni hatua muhimu ya kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Samia katika kutuletea maendeleo,"amesema Kiboye.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news