Na Yusuph Mussa, Korogwe
Mwenyekiti Mstaafu wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Hillary Ngonyani amefariki dunia.
Ngonyani amefariki dunia leo Septemba 9, 2021 saa 9.15 alasiri akiwa nyumbani kwake Mtaa wa Memba mjini Korogwe ikiwa ni katika jitihada za kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa mmoja wa watoto wake, Richard Ngonyani, anasema mzee Ngonyani alikuwa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga hadi asubuhi ya leo akiwa anasumbuliwa na Nimonia.
Na tayari saa nne asubuhi ya leo walikuwa wamekamilisha rufaa hiyo ikiwa tayari pia wamepata gari la wagonjwa (Ambulance), hivyo wakamtoa Magunga na kumpeleka nyumbani kwake kwa ajili ya maandalizi ya kwenda Muhimbili.
Richard anasema mara ghafla wakaona amezidiwa na kufariki saa 9.15 alasiri.
Mzee Ngonyani amekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Korogwe mwaka 2000 hadi 2005 mji huo ulipopandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji Korogwe mwaka 2004.
Ngonyani amekuwa Diwani wa Kata ya Kwamndolwa tangu mwaka 2000 hadi mwaka 2020 baada ya kushindwa na Neema King'oso kwa kura nne kwenye uchaguzi wa kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM), ambapo Neema alipata kura 42, huku yeye akipata kura 38.
Ngonyani ambaye ni kaka wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini marehemu Stephen Ngonyani maarufu kama Majimarefu, alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe kwa miaka 10 tofauti.
Alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe 2005-2010, Kabla ya kuangushwa na Angelo Bendera, aliyekuwa Diwani wa Kilole. Lakini alirudi tena kwenye kiti hicho mwaka 2015 hadi 2020.
Taarifa za msiba, wapi atazikwa, na lini, zitatolewa baadae. SOTE NI WA MUNGU NA KWAKE TUTAREJEA.