NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Siku chache baada ya Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa wa Kanisa la Penuel Healing Ministry la Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam, Alphonce Temba kutabiri kuhusu ushindi wa Chama cha Upinzani cha United Party for National Development (UPND) kushinda urais kutimia na kuwa miongoni mwa wageni walioshiriki hafla ya kuapishwa kwa Rais, leo ameitwa tena Zambia.
Agosti 24, mwaka huu, Mwinjilisti Temba alikuwa ni miongoni mwa wageni maalum walioudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Zambia, Hakainde Hichilema jijini Lusaka. Rais huyo ameahidi kuujenga upya uchumi wa nchi hiyo ambao unaoyumba na kupunguza umaskini.
Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa wa Kanisa la Penuel Healing Ministry la Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam, Alphonce Temba (wa pili kulia), akiwa na viongozi wa
Kamati ya Viongozi wa Dini pamoja na chama tawala, kushoto ni Mchungaji Kelly Mukonka ambaye ni Mwenyekiti wa kamati, anayefuata ni Mwenyekiti wa chama tawala, Stephen Katuka na kulia ni Katibu wa kamati, Mtume Richard Mubanga wakiwa katika picha ya pamoja leo Septemba 2, 2021 jijini Lusaka, Zambia.
Mwinjilisti Temba ambaye alikuwa anaendelea na ziara zake za kuhubiri injili katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara akiwa mjini Gaborone, Botswana alipewa wito maalum na chama tawala ikiwa ni mwendelezo wa mipango ya kulifanya Taifa hilo la Zambia kumtegemea Mungu zaidi ili aweze kuponya majeraha ya kiuchumi wanayopitia ukiwemo umaskini.
Baada ya kufika ofisi za chama tawala leo Septemba 2, 2021 ambapo Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa Alphonce Temba alikuwa amepangiwa kukutana na Kamati ya Viongozi wa Dini iliyopo kisheria kumshauri Rais walikaa na kujadili mambo mbalimbali.
Aidha, baada ya ujumbe wa kamati hiyo kumsikiliza Mwinjilisti Temba kama anao uwezo wa kuwa anaitwa rasmi kwa ajili ya mashauri ya kiroho kwa Rais, kwa umoja wao waliridhia kutokana na karama iliyopo ndani yake.
Hivyo,baada ya Mwenyekiti wa chama tawala Zambia, Stephen Katuka kumpendekeza jina lake kamati imekubaliana naye kuwa Mwinjilisti wa Kimataifa Alphonce Temba kwanza ni mpakwa Mafuta ya Mungu kwa watawala na amebeba neema ya tofauti na nguvu za Mungu si kwa Zambia tu bali kwa mataifa mbalimbali duniani, hivyo atakuwa miongoni mwa watumishi wa Mungu ambao watakutana na rais kwa kumuombea na kumshauri.
Kutokana na hatua hiyo,kamati imeagiza ndani ya siku mia moja za uongozi wa Mheshimiwa Rais Hakainde Hichilema atakutanishwa naye na kufanya maombi ndani ya Ikulu ya Zambia kadri Mungu atakavyomuongoza.
Aidha, kwa sasa taratibu zinaendelea za kumjulisha rais ingawa jambo la kushangaa kamati hiyo ambayo inaanda maombi ya kitaifa ya kumshukuru Mungu yatakayofanyika Septemba 12, 2021 ambayo yatafunguliwa na Mheshimiwa Rais Hakainde Hichilema kwa taifa zima kumshukuru Mungu kwa zoezi lote kwenda vizuri wamesema Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete lazima aalikwe.
Katika majadiliano yao wamesema kuwa, wanapenda kumwalika Mheshimiwa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimamia uchaguzi kama mwangalizi na kushauri viongozi wa Zambia kwa hekima na busara kubwa.
Wanasema, wanaamini Mheshiwa Kikwete alifanya kazi kubwa mno mpaka kukawa na utulivu uliopo sasa nchini Zambia, hivyo ataendelea kuwa nguzo muhimu katika mustakabaliwa amani ya Zambia.
Hata hivyo, Mwinjilisti wa Kimataifa Alphonce Temba baada ya kutembelea nchi mbili za Botswana na Zambia ambapo pia wachungaji wengi wamempa mialiko katika nchi hizo hila kwa kuwa alikuwa na ujumbe maalumu wa ki-Mungu alishindwa kukubaliana nao badala yake ametoa wito kwa mataifa mbalimbali kutambua kuwa, hiki ni kipindi cha kutubu na viongozi wakuu wa nchi kumruhusu Mungu, kwani majanga hayataisha bila Mungu kuingilia.
Huku akitolea mfano nchi ya Botswana iliyofungia wananchi na kuwalisha na inayo uwezo wa kuwalisha kwa zaidi ya miaka mitano bila kufanya kazi, lakini ndiyo nchi inayoongoza kwa vifo vya Corona Duniani.
Pia amezungumzia safari yake ya kuingia Botswana namna ambavyo ilikuwa ya kimiujiza maana nchi bado imefungwa na wasafiri wanaopita kwenda Afrika Kusini, ndiyo wanaoruhusiwa sana kupita kila baada ya siku tatu na unapaswa kupimwa na gharama zake ni Pula 500 ambazo ni karibu laki moja ya kitanzania.
Pamoja na kuomba kibali cha wiki moja au mbili mpakani, ila alishangaa ofisa wa uhamiaji akimpa muda wa miezi miwili kukaa nchini.
"Pia natoa wito kwa watumishi wa kweli wa Mungu kuwa sasa ndiyo kipindi cha kulihubiri neno la Mungu na majanga ni moja ya vitu vinavyo wafanya watu kuingiwa na hofu na kujikuta wakimpokea Bwana Yesu katika maisha yao,"amesema Mwinjilisti Alphonce Temba.