Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog
Diwani wa Kata ya Nyasho ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Musoma, Haji Mtete pamoja na Kamati ya Siasa ya Kata ya Nyasho wamefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata hiyo iliyotekelezwa kuanzia mwezi Januari hadi Juni na kubaini miradi hiyo kutekelezwa kwa ufanisi.

Ziara hiyo imefanyika Septemba 9, 2021 ambapo Wajumbe wa kamati hiyo walifika katika Shule ya Sekondari Nyasho na kupokea taarifa ya ujenzi vyumba viwili vya maabara ya Biolojia na Kemia ambavyo vipo katika hatua ya mwisho kuanza kutumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kufuatia Serikali kuu kutoa shilingi milioni 30 kumalizia ujenzi wa vyumba hivyo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyasho, Matiko Seruka ameieleza kamati hiyo kuwa, walipokea fedha Shilingi Milioni 30 kutoka Serikali Kuu ambazo zimefanya kazi mbalimbali za ukamilishaji wa vyumba viwili. Na kwa sasa kilichobakia ni uwekaji wa umeme na maji katika vyumba hivyo na baada ya hatua hiyo, wataomba vifaa serikalini ili wanafunzi waanze kutumia maabara hizo.
"Tuzilipata fedha kutoka Serikali Kuu kutokana na maboma kuwa tayari baada ya Wananchi kuchangia, tupo kwenye hatua ya kuomba vifaa ili shughuli ya utumiaji wa maabara hizi uanze kufanyika. Hii ni hatua kubwa sana ujenzi wa maabara hizi kufikia kiwango kizuri cha ukamilifu,"amesema Matiko.



Diwani wa Kata ya Nyasho, Haji Mtete amepongeza juhudi za Wananchi wa kata hiyo waliochangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyumba hivyo vya maabara na kuiwezesha Serikali kuleta fedha ambazo zimewezesha ukamilishaji wake. Huku akiwaomba pia kuendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo pasipo kusukumwa na serikali.
Pia, Mtete amewahakikishia Wananchi wa Kata ya Nyasho kuwa, ataendelea kuwapa ushirikiano wa dhati na kuwatumikia kuwaletea maendeleo na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ufanisi unaotakiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Nyasho, Fidelisi Manyerere akizungumza na Walimu wa Shule ya Sekondari Nyasho, amewataka walimu wa shule hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanafanya vizuri katika masomo yao.






Aidha, kamati hiyo pia imefanya ukaguzi wa madaraja mawili ya Nyakisaka yaliyopo ndani ya Kata ya Nyasho ambayo ni muhimu kwa shughuli za maendeleo ndani ya kata hiyo.