Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaendelea kuonyesha mfano kwa wengine kupitia mazoezi jumuishi

Na Veronica Mwafisi-DODOMA

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael amesema tangu watumishi wa ofisi yake waanze utaratibu wa kufanya mazoezi ya pamoja mara moja kwa wiki yameongeza kasi ya watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kutokana na afya zao kuimarika kupitia mazoezi hayo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (Wa kwanza kushoto) akishiriki kufanya mazoezi ya viungo wakati wa mazoezi ya watumishi wa ofisi yake yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Dkt. Michael aliyasema hayo jana wakati wa mazoezi ya watumishi wa ofisi yake yaliyoongozwa na Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Dkt. Laurean Ndumbaro katika Ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Kutokana na mazoezi wanayofanya, watumishi wamekuwa familia moja hivyo wameongeza wigo wa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuimarisha kinga ya miili yao dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, Dkt. Michael amefafanua.

Aliongeza kuwa, mazoezi yamewawezesha watumishi wa ofisi yake kuwa na afya njema, kuipa mwili yao nguvu na afya ya akili inayowawezesha kutekeleza majukumu yao bila uchovu wa aina yoyote.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akisisitiza ufanyaji wa mazoezi kwa watumishi wa ofisi yake wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Kutokana na faida hiyo waliyoipata kupitia mazoezi, Dkt. Michael, amewahimiza watumishi wa ofisi yake kuendelea kufanya mazoezi ili kuendelea kuimarisha afya zao kwa ajili ya kuongeza ufanisi kiutendaji.

Akizungumzia faida waliyoipata kupitia mazoezi, mmoja wa watumishi wa ofisi hiyo Bi. Elizabeth Fusi amesema, mazoezi yamemsaidia sana kuimarisha afya yake na kuongeza kuwa amefurahia sana mchezo wa kukimbiza kuku.

Nimekuwa mshindi katika mchezo wa kukimbiza kuku na kupewa zawadi hivyo, naushukuru uongozi wa ofisi yangu kwa kuhamasisha mazoezi kwa watumishi, mazoezi ambayo yamesaidia kuongeza ufanisi kiutendaji, Bi. Fusi amefafanua.

Kwa upande wake, mtumishi mwingine Bw. George Kapera amesema kuwa, mazoezi yanazidi kuimarisha afya zao pamoja na utendaji kazi wao na kuongeza kuwa amefurahi kucheza mchezo wa kukimbiza kuku pamoja na kukimbia na gunia.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya mazoezi ya viungo ili kuimarisha afya zao wakati wa mazoezi ya watumishi wa ofisi hiyo yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakijiandaa kushindana kukimbia na magunia wakati wa mazoezi ya watumishi wa ofisi hiyo yalifanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya mazoezi ya kuimarisha afya zao katika Ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa nyakati tofauti wameushukuru uongozi wa ofisi yao kwa kuweka utaratibu endelevu unaowapa fursa ya kufanya mazoezi ya pamoja kila Ijumaa ya wiki yenye lengo la kuimarisha afya zao na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news