NA MWANDISHI MAALUM
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa anawatahadharisha wananchi kuwa makini na matapeli wanaotumia akaunti za kughushi za mitandao ya kijamii kwa kutumia jina lake ili kuwapatia ajira.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 15,2021 kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Ofisi ya Rais-Utumishi, Bi.Mary L. Mwakapenda.
Kwa sasa matapeli hao wametengeneza akaunti ya facebook inayosomeka kwa jina la Mohamed Mchengerwa inayoonyesha Mhe. Mchengerwa akiwasiliana na wananchi kwa lengo la kuwapatia ajira katika Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA).Mhe. Mchengerwa anawasisitiza wananchi kuwa makini na matapeli hao kwani suala la kupata ajira lina taratibu zake ambazo hazihusishi mawasiliano ya kwenye mitandao.Hivyo, anauarifu umma kuwa akaunti inayotumika katika vitendo hivyo viovu sio yake bali kuna watu wenye nia ovu wanaotaka kumchafua yeye pamoja na Serikali.Aidha, Mhe. Mchengerwa anatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za matapeli hao kwenye ofisi yake na vyombo vya dola ili zisaidie kukabiliana na tatizo hilo.Sambamba na hilo, Mhe. Mchengerwa anawaonya matapeli hao kuacha tabia hiyo kwani Serikali kupitia vyombo vya dola inaendelea kufuatilia nyendo zao ili kuwabaini na kuwachukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.