NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein
Ali Mwinyi leo ameongoza maziko ya Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Jaji
Haji Omar Haji yaliyofanyika Shakani, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja,
Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiweka mchanga katika kaburi la Marehemu Jaji ya Mahakama Kuu Zanzibar, Haji Omar Haji, maziko yaliofanyika katika Kijiji cha Shakani Wilaya ya Magharibi ‘B’Unguja leo Septemba 12, 2021.(Picha na Ikulu).
Viongozi
mbalimbali wamehudhuria katika maziko hayo akiwemo Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman
Makungu pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa, dini na serikali,
wananchi na wanafamilia.
Mapema
Alhaj Dkt. Mwinyi alijumuika pamoja katika hitma na sala ya kumsalia
Marehemu Jaji Haji Omar Haji huko katika Masjid Noor, uliopo Kombeni,
Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi sala ambayo
iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh, Saleh Omar Kabih.
Akisoma
Wasifu wa Marehemu Jaji Omar Haji, mara baada ya maziko ya Marehemu,
Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed amesema kuwa,
Marehemu amezaliwa Aprili 04, 1967 huko Wilaya ya Mafia katika Mkoa wa
Pwani, Tanzania Bara.
Amesema
kuwa, Marehemu ameanza Elimu yake ya Msingi kuanzia darasa la Kwanza
hadi darasa la Saba mwaka 1978 hadi 1984 huko Mafia na mnamo mwaka 1985
alihamia Zanzibar na kujiunga katika Skuli ya Msingi Kiembesamaki kwa
kuendelea na elimu yake hadi mwaka 1987.
Kwa
mujibu wa maelezo ya Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, Mnamo mwaka
1988 hadi 1991 Marehemu alianza Elimu yake ya Sekondari katika Skuli ya
Vikokotoni, na kuendelea na masomo yake ya Kidato cha Tano na Sita mnamo
mwaka 1993 hadi 1995 katika Skuli ya Sekondari ya Lumumba.
Mwaka
1997 hadi mwaka 1999 Marehemu alijiunga na Chuo cha Mzumbe kwa masomo
ya Stashahada ya Sheria na mwaka 2000 hadi 2004 alijiunga na Chuo
Kikuu cha Zanzibar (ZU) na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria na
mnamo mwaka 2008 alisoma Shahada ya Uzamili ya Sheria katika Chuo Kikuu
cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini.
Akimuelezea
katika nafasi zake za kazi alizopitia Marehemu Haji Omar Haji, Mrajis
wa Mahkama Kuu Zanzibar alieleza kwamba Marehemu aliwahi kuwa Mwalimu wa
muda katika skuli ya Sekondari ya Haile Sellasie na mnamo Oktoba 1996
aliajiriwa kazi na kuanza akiwa Karani wa Mahkama Kuu Zanzibar.
Marehemu
aliwahi kuwa Hakimu wa Mkoa katika Mahakama ya Mkoa Vuga mnamo mwaka
2005 hadi 2008 wakati akiwa Hakimu wa Mkoa alipata nafasi ya kufundisha
katika Chuo cha Azania.
Marehemu
Haji Omar Haji aliteuliwa kuwa Naibu Mrajis Mahakama Kuu Pemba mnamo
mwaka 2009-2011 na mnamo Julai 04,2018 hadi Februari 01,2021 alifanya
kazi katika Mahkama ya Afrika Mashariki akiwa ni Mtendaji Mkuu wa
Mhakama hiyo.
Aidha,
mmano Februari 01, 2021 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi alimteua kuwa Jaji wa Mahakama
Kuu Zanzibar na kuapishwa Februari 2021 na mnamo Agosti 16,2021 Jaji
Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alimteua kuwa Jaji Mkaazi Pemba.
Marehemu Haji Omar Haji, hadi umauti unamfika alikuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar na Jaji Mkaazi Pemba.
Marehemu
Jaji Haji Omar Haji amefariki jana Septemba 11,2021 katika Hospitali ya
Rufaa Mnazi Mmoja baada ya kuugua kwa muda mfupi, marehemu ameacha
Kizuka Mmmoja na watoto 4, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala
pema peponi, Amin.