Rais Samia afanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu UN

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 11 Septemba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bi. Amina J. Mohammed, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Bi. Amina amewasilisha salamu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na kumpongeza Mhe. Rais Samia kwa kushika nafasi ya Urais na kumtakia heri katika majukumu yake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bibi Amina J. Mohammed wakati Bibi Amina alipofika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma leo Septemba 11, 2021. (Picha na Ikulu).

Mhe. Amina amemuhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kumuunga mkono katika jitihada zake mbalimbali za kuiletea maendeleo Tanzania , ikiwemo kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Aidha, amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada anazochukua dhidi ya janga la UVIKO 19 ambapo amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kuhakikisha kuwepo na usawa wa upatikanaji wa chanjo na wanaendelea na majadiliano na Taasisi za Kifedha kuona ni jinsi gani zinasadia nchi zinazoendelea kukabiliana na ugonjwa huo.

Vilevile, ameahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amempongeza Mhe. Amina kwa kuteuliwa tena kushika nafasi hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kumhakikishia ushirikiano zaidi kwa kuwa Umoja wa Mataifa kupitia taassisi zake mbalimbali ni mbia wa maendeleo nchini.

Mhe. Rais Samia amemueleza Mhe. Amina kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini ambapo katika kipindi cha miezi mitatu idadi ya wawekezaji imeongezeka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news