Na Mwandishi Maalum, New York
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewasili nchini Marekani kuhudhuria Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JF Kenedi Jijini New York Marekani leo Sept 19,2021 kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UN unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 Sept 2021. (Picha na Ikulu).
Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili mjini New York, Marekani leo tarehe 19 Septemba, 2021 kuhudhuria Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Baada ya kuwasili Jijini New York, leo Jumapili Septemba 19, 2021, Rais Samia amepokelewa na Watanzania wanaoishi nchini humo na kuwashukuru kwa mapokezi makubwa waliyomuonesha.
Rais Samia amewafahamisha watanzania hao kuwa yeye na ujumbe wake mbali na kuhudhuria Mkutano huo pia atahudhuria mikutano mbalimbali itakayojadili masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba dunia, Rais Samia amesema Tanzania haijaathirika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mataifa mengine kufuatia kuwepo kwa mipango mbalimbali ya kukabiliana na athari za mazingira nchini Tanzania.