Na Nuru Mwasampeta-WM
Ombi la wafanyabiashara wa Tanzanite kusalia na kuuza madini yao popote duniani limekubaliwa na Serikali kwa sharti la kuhakikisha wanatoka na madini nje ya ukuta baada ya kujaza fomu maalum yenye taarifa ya kiasi cha madini hayo yakiwa yamelipiwa kodi stahiki za Serikali.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko akizungumza na wananchi wa Simanjiro mkoani Manyara (hawapo pichani) alipokutana nao mwishoni mwa wiki, amesema nia ya Serikali ni kuwaendeleza na kuwafanya wachimbe kwa tija.
Awali walikuwa wakiyarejesha ndani ya ukuta ili kuhifadhiwa
baada ya kukosa wanunuzi wa madini hayo jambo ambalo lilikuwa
likilalamikiwa na wachimbaji hao kwa kutaka kuyahifadhi wao wenyewe
pamoja na kuruhusiwa kusafirisha popote duniani ili kutafuta wateja.
Kibali
hicho kimetolewa na Serikali kupitia Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko
mwishoni mwa wiki alipofanya kikao na wachimbaji na wafanyabiashara wa Tanzanite ndani ya ukuta wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro mkoani
Manyara.
Dkt. Biteko alitoa kibali mara baada ya Mbunge wa
Simanjiro, Christopher Ole Sendeka kuwasilisha ombi hilo pamoja na
mengine kwa niaba ya wananchi, wafanyabiashara na wachimbaji wa Tanzanite.
Aidha, Dkt. Biteko aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa
tanzanite kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya
barabara hususani barabara zinazoelekea sehemu zao za machimbo na
kueleza kuwa Wizara yake itatafuta namna ya kushiriki katika kuboresha
barabara kubwa kama ilivyoombwa na wananchi wa eneo hilo.
Pamoja
na hayo, Dkt. Biteko aliendelea kuwataka wachimbaji na wafanyabiashara
wa madini kupendana na kuacha vitendo vya chuki miongoni mwao ili
kuifanya Sekta ya Madini kuendelea kukua na kuongeza mchango wake kwenye
uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake,
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere aliishukuru Wizara ya Madini
na kubainisha kuwa imekuwa msaada sana katika kuwawezesha kutekeleza
majukumu yao.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko (kulia) akisikiliza kwa makini hoja zinazowasilishwa kwake na Mbunge wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa tanzanite Mirerani alipokutana nao kusikiliza na kutatua kero zao, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole
Sendeka aliwasilisha maombi ya wananchi wa Wilaya hiyo ikiwa ni pamoja
na wachimbaji wa tanzanite kuruhusiwa kujaza fomu maalumu ya madini
waliyonayo na kwenda kuyauza nje ya Mirerani tofauti ilivyokuwa ambapo
walikuwa wakiwauzia wanunuzi (brokers) waliopo ndani ya ukuta kwa bei
ya kutupwa.
Alisema, kufanyiwa kazi kwa ombi hilo kutaondoa
ukiritimba kwa baadhi ya wanunuzi wanaonunua tanzanite kwa bei ya
kutupwa na hivyo kuwafanya wachimbaji wa tanzanite kunufaika na madini
wanayopata.
Pamoja na ombi hilo, Sendeka aliwasilisha ombi la kutengenezewa barabara yenye urefu wa kilomita 5 inayoingia na kutoka nje ya ukuta katika eneo tengefu la mirerani kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za usafiri hususani msimu wa mvua ombi lililoahidiwa kufanyiwa kazi na serikali baada ya kukamilika kwa mchakato wake .
Dkt. Biteko alikuwa na ziara ya siku mbili katika eneo tengefu la Mirerani ambapo alieleza kauli ya Serikali juu ya utekelezaji wa maagizo ya kufanyika kwa biashara ya tanzanite katika mji huo wa Mirerani mkoani Manyara.