NA HADIJA BAGASHA
Wananchi wa kijiji cha Muhuwesi kata ya Muhuwesi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wamemshukuru mwekezaji Ruby International Ltd kwa kuwajengea zahanati ya kisasa ambayo itawasaidia kupata huduma bora za afya.
Aidha,wananchi hao wamemuomba mwekezaji kuendelea kuwajengea miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu na miundombinu mingine kwani uwezo wa kufanya hayo anao.
Wakiongea kwa nyakati tofauti Salim Nampipiru ambaye ni mwakilishi wa wazee wa kijiji hicho amesema wawekezaji wa madini wamepita wengi katika kijiji hicho, lakini hawakufanya maendeleo kama hayo hivyo aendelee kuwa mwokozi wa kijiji kwa kipindi hiki.
Naye Bi.Hamida Selemani amesema yeye kama mwanamke kwa niaba ya wenzake anaishukuru kampuni ya Ruby kwa kuwavika nguo wanawake kwani walikuwa wanadhalilika nyakati za kujifungua hapo nyuma.
Iman Ngonyani ni Diwani wa Kata ya Muhuwesi amewaomba wananchi kuendelea kumlinda na kumpa sapoti mwekezaji ili awe na moyo wa kuendelea kukisaidia kijiji chao kauli ambayo imeungwa mkono na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Sizza Marandu ambapo amesema ni wawekezaji wachache wanaokumbuka kufanya maendeleo katika vijiji wanavyowekeza.
Salim Alaudin Hasham ndiye mkurugenzi wa Ruby International Ltd ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa wananchi na kwa kipindi chote atakachokuwepo kijijini hapo ataendelea kusaidia mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
Kijiji cha Muhuwesi kimekuwa maarufu kutokana na kutoa madini ya vito yenye thamani kubwa ambayo yanatoka kwenye Mto Muhuwesi unaopita kwenye kijiji hicho.