Serikali yatoa tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa

NA MWANDISHI MAALUM- WAMJW

Katika kuadhimisha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 28 ya kila mwezi Septemba, Wizara ya Afya imewatahadharisha wananchi kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao unaweza kusababisha vifo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa Yasiyo ambukiza Dkt. James Kiologwe akitoa Tamko la Serikali kwa niaba ya Katibu Mkuu katika kuadhimisha siku ya ugonjwa huo Duniani.

“Kwa mwaka huu kati ya mwezi Januari hadi Agosti, watu 39,787 wametolewa taarifa ya kung’atwa na mbwa au wanyama wa jamii hiyo ikiwa ni ongezeko la zaidi ya watu 5,000 ukilinganisha na kipindi kama hicho cha mwaka uliopita” amesema Dkt. James Kiologwe na kuendelea kusema kuwa takwimu hizo hazijumuishi matukio yaliyotokea katika vituo vya kutolea huduma bila kutolewa taarifa au yaliyotokea nyumbani na waathirika ambao hawakufika katika vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo tatizo hilo ni linaweza kuwa kubwa kuliko tunavyofikiri,” amefafanua zaidi Dkt. James Kiologwe.

Ameitaja Mikoa inayoongoza kuwa ina idadi kubwa ya wagonjwa kuwa ni Mkoa wa Morogoro ambao una wagonja 4329 ukifuatiwa na Mkoa wa Dodoma wenye wagonjwa 4233.

“Waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto chini ya miaka 15 na hii inaweza kuwa ni kwa sababu wao ndio wanaokuwa karibu na mbwa (anayefugwa) muda mwingi, na pia hupenda kucheza au kuchokoza mbwa wasiowafahamu njiani” amesema Dkt. Kiologwe.

Dkt. James amesema kuwa Ugonjwa wa kichaa cha mbwa husababishwa na Kirusi wa Kichaa cha Mbwa (Rabies Virus) kutoka kwa wanyama jamii ya mbwa ambao wameathirika na kirusi hiki (Mbwa, paka, mbweha, fisi na wengineo) na humwingia mwanadamu kupitia mate ya mnyama huyo kuingia katika jeraha na dalili huanza kuonekana baada ya kuathirika kwa mfumo wa kati wa fahamu, ambazo ni pamoja na kuwashwa sehemu ya jeraha, homa, kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, kuogopa maji na mwanga, kutokwa mate mengi mfululizo, kuweweseka (kushtuka mara kwa mara na kuogopa), kupooza na hatimae kupoteza maisha. Wakati mwingine watu huhusisha dalili hizi na imani potofu za kishirikina.

“Endapo mtu ameng’atwa na mbwa, hatua ya kwanza muhimu ni kuosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririkika na sabuni. Kidonda kisifungwe na kisha apelekwe au afike haraka katika kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata chanjo ya kuzuia kichaa cha mbwa,”amesema Dkt. James Kiologwe.

Amesisitiza kuwa, ni muhimu aliyeng’atwa na mbwa afanyiwe tathmini ya kina katika kituo cha kutolea huduma ili aweze kupatiwa chanjo kamili na iwapo chanjo itatolewa ni budi kumaliza kozi zote za chanjo. 

Ameendela kusema kuwa, wanyama jamii ya mbwa, paka wasiruhusiwe kulamba vidonda, kwani mate yao huweza kuleta maambukizi endapo wameathirika, huku Wamiliki wa mbwa wahakikishe wanachanja mbwa wao dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa mara moja kila mwaka na kupata cheti. 

Amesema kuwa mbwa wafungiwe ndani wakati wa mchana na wasiachwe kuzurura hovyo, kwani wanaweza kupata maambukizi endapo watakutana na mnyama aliyeambukizwa pamooja na kuhakikisha mazingira yote ni safi, ili kutowapa chakula mbwa wanaozurura mtaani na kuzoea kuja katika mazingira tunayoishi.

Ametoa rai kwa wazizi kutoa elimu kwa watoto na kuwakataza kuchokoza mbwa wasiowajua (mfano: kuvuta mkia au masikio, kumpanda mgongoni).

Amesema kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikia na sekta nyingine ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM) - Dawati la Afya Moja pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Chakula Duniani (FAO) pamoja na wadau mbalimbali wamefanya juhudi mbalimbali za kudhibiti ugonjwa huo na kuhakikisha inapunguza ukubwa wa tatizo linalohusiana na ugonjwa huo kwa; Kutoa elimu kwa umma; Kuboresha dhana ya Afya Moja nchini; Kurahisisha upatikanaji wa huduma ya chanjo ya Kichaa cha Mbwa kwa wananchi; Kurahisisha upatikanaji wa huduma ya chanjo kwa kwa wanyama hasa mbwa.

“Serikali inatambua gharama kubwa za upatikanaji wa chanjo, hata hivyo kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na sekta nyingine imeweza kuchangia gharama za upatikanaji wa chanjo ili ziwafikie wananachi kwa gharama wanazoweza kumudu,” amesema Dkt. James Kiologwe.

Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kutekeleza mikakati na juhudi za pamoja za sekta zote zinazohusika kudhibiti ugonjwa huo inaandaa ‘Mkakati wa Kudhibiti Kichaa cha Mbwa’ wenye lengo la kutokomeza ugonjwa huu ifikapo 2030.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news