Na Anneth Kagenda
JAMII imetakiwa kuhakikisha inawasaidia watoto yatima nchini hasa wale wanaolelewa katika vituo vya kulea watoto katika maeneo mbalimbali kwa madai kuwa kujitolea kuwasaidia watoto wadogo ni thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Hayo
yamesemwa Dar es Salaam na Uongozi wa Taasisi ya Al - Wadoud yenye
makazi yake nchini Omany kupitia kwa Mwenyekiti wake Sheikh Abdul Qader
Al Jahdhamy, pamoja na Uongozi wa Tanzania Peace Foundation (TPF-TY),
kupitia kwa Mwenyekiti wake Edward Mwenisongole wakati wakikabidhi msaada
wa vyakula kwa Kituo cha kulelea watoto Yatima cha Maunga Orphanage
Centre kilichopo Kinondoni Mkwajuni chenye watoto zaidi ya 48.
Mwenyekiti
Sheikh Al Jahdhamy amesema kuwa, ni wakati mwafaka kwa jamii mzima
kuhakikisha wanawasaidia watoto yatima na hasa wale walioko kwenye vituo
vya kulelea yatima kwani kufanya hivyo ni kupata dhawabu kwa Mungu.
"Lakini pia ijulikane kwamba suala lingine ni kwamba watoto hawa ndio Taifa na viongozi wajao, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake kwenye jamii hana budi kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto hawa,"amesema Kiongozi huyo.
Naye Mwenyekiti Edward Mwenisongole amesema, taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kuhubiri amani kwa Taifa la Tanzania na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa kupendana.
"TY Mkoa tunalojukumu kubwa la kueneza upendo na amani kwenye nchi yetu na pia suala la kuwasaidia na kuwalea watoto yatima ni la kwetu, hivyo watoto hawa wakikosa amani ni moja ya sababu inayoweza kupelekea pia kuwepo kwa vurugu hivyo jamii tunatakiwa kushirikiana,"amesema Mwenyekiti Mwenisongole.
Mwanzilishi wa Kituo hicho Zainabu Maunga, alitoa shukrani zake za dhati kwa uongozi mzima wa TPF, TY ,TW na Uongozi wa Taasisi ya Al- Wadoud kwa msaada huo mkubwa kwa watoto wake ambao alisema kuwa kwa kiasi kikubwa utawasajdia watoto hao.
Amesema pamoja na mambo mengine kituo chake kimekuwa kikikabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni bili za umeme, maji uhaba wa vyakula na kwamba anatamani watoto hao wangejengewa kituo kikubwa cha kulelea watoto hao.
"Nashukuru sana kwa misaada hii kutoka kwenye taasisi zote lakini niiombe jamii iendelee kujitolea kuwasaidia watoto hawa kwani mnawaona walivyokuwa wadogo na wanatakiwa mahitaji mbalimbali,"amesema Bi Zainabu.