TEA kusimamia uanzishwaji wa uhuishaji wa mifuko ya elimu ya halmashauri

Na Eliafile Solla, TEA

Miundombinu bora ya elimu katika halmashauri nyingi hapa nchini ni changamoto kubwa ambayo haiwezi kuachiwa Serikali peke yake, bali kuna haja ya kuongeza ushirikiano wa jamii katika kutatua changamoto hizo.

Kauli hii imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi Bahati. I. Geuzye, alipokuwa akitoa nasaha zake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi. Bahati. I. Geuzye akiwasilisha nasaha zake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati. I. Geuzye (katikati) akiwa amezungukwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) wakichukua mawasiliano yake mara baada ya kutoa nasaha zake kwa wajumbe hao jijini Dodoma.

Awali ya yote Bi. Bahati alibainisha kwamba, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inatambua umuhimu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika kuhamasisha na kuboresha mahusiano yao ya kiutendaji na Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji kote nchini.

‘‘Kutokana na changamoto hizo za miundombinu bora ya elimu, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo inaratibu na kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeandaa utaratibu utakaowezesha Halmashauri zetu kuanzisha Mifuko ya Elimu na kwa zile Halmashauri ambazo tayari zina mifuko hiyo tuna dhamira ya kuihuisha na kuanza kuitumia kikamilifu’’, alisema Bi. Bahati.

Aliongeza kwamba, katika mwaka 2020 sheria ndogo ya uanzishwaji wa Bodi ya Mfuko wa Elimu wa Halmashauri iliridhiwa na Mhe. Waziri mwenye dhamana wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na vile vile mwongozo wa uanzishwaji wa Mifuko umekwishaandaliwa na kusambazwa kwa wajumbe hao wa mkutano wa ALAT.
Bahati Geuzye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Bi. Gimbana Ntavyo, mara baada ya kutoa nasaha zake kuhusu uanzishaji na uhuishaji wa Mifuko ya Elimu ya Halmashauri katika Mkutano Mkuu wa ALAT wa mwaka jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), wakipata elimu kuhusu Mfuko wa Elimu wa Taifa na uanzishwaji wa Mifuko ya Elimu ya Halmashauri katika banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) jijini Dodoma.

‘‘Kazi iliyopo mbele yetu ni kutekeleza lengo kuu la kuanzisha na kuhuisha Mifuko ya Elimu katika Hamlashauri zote nchini, moja ya mipango inayolenga uboreshaji wa elimu katika maeneo wanayoishi wananchi’’ alibainisha Bi. Bahati

Zoezi hili la uanzishwaji na uhuishwaji wa Mifuko ya Elimu ya Halmashauri lina faida nyingi ikiwemo kuwezesha Halmashauri kukuza ushirikiano wa jamii katika kuchangia miradi ya kipaumbele ya elimu; kuboresha, kuendeleza na kukuza viwango vya elimu katika Halmashauri husika.

Vile vile mifuko hii itawezesha Halmashauri kutenga sehemu ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya miradi ya elimu ndani ya Halmashauri pamoja na kuratibu upatikanaji wa michango kutoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kiserikali, mashirika ya kidini na watu binafsi kwa ajili ya kusaidia uendelezaji wa miradi ya elimu ndani ya Halmashauri hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news