TPA, MSCL zatakiwa kuandaa maegesho ya Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu

Na Deniza Cyprian-WUU

Serikali imeiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuandaa miundombinu ya maegesho ya meli kwa ajili ya meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” inayojengwa katika Bandari ya Mwanza.Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Philemon Bagambilana, wakati akikagua mradi wa ujenzi wa Meli Mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” jijini Mwanza.

Akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa meli hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kuwa kazi za ujenzi wa meli hiyo kwa sasa zimefikia asilimia 53.8 na ifikapo mwezi Aprili, 2022 meli hiyo itaingizwa majini kwa mara ya kwanza na kuendelea kumaliziwa ujenzi wake ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2022 na baadae kufanyiwa majaribio na kukaguliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kabla ya kuanza kutoa huduma.

“Meli hii ni kubwa kuliko meli zote zinazofanya safari katika Ziwa Victoria kwani ina urefu wa mita 92.6, upana mita 17 na kimo mita 20, hivyo MSCL kwa kushirikiana na TPA hakikisheni miundombinu ya maegesho kwa ajili ya meli hii inaboreshwa ili meli itakapokuwa tayari iweze kuanza kazi mara moja kwani meli hii ni inatarajia kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma za usafiri wa maji katika Ziwa Victoria” amesema Kasekenya. Meneja wa mradi wa ujenzi wa Meli Mpya ya MV MWANZA ‘Hapa Kazi Tu’ kutoka Jeshi la Wanamaji Tanzania, Eng. Elias Kivara, akitoa taarifa ya mradi kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya (wa pili kushoto), wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo ambayo utekelezaji wake umefikia asililimia 53.8, jijini Mwanza.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Philemon Bagambilana, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, hatua za ujenzi wa Meli Mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu”, jijini Mwanza.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Philemon Bagambilana amemueleza Naibu Waziri Kasekenya kuwa ujenzi wa meli ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” unagharimu dola za kimarekani milioni 39 sawa na shilingi Bilioni 89.7 na umeenda sambamba na ujenzi wa chelezo kipya kinachotumika kwenye ujenzi wa meli hiyo ambacho pia kimegharimu dola za Kimarekani milioni15.

Bw. Bagambilana ameongeza kuwa Kampuni yake imekwishakamilisha ukarabati wa meli ya “New Victoria Hapa Kazi Tu” kwa gharama ya Shilingi Bilioni 25.5 na “New Butiama Hapa Kazi Tu” kwa Shilingi Bilioni 5.7 na tayari meli hizo zinaendelea kufanya kazi katika Ziwa hilo.
Kaimu Meneja wa Bandari Ziwa Victoria, Bw. Vicent Steven, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wakati akikagua hatua za ujenzi wa Meli Mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu”, jijini Mwanza.
Kaimu Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Eng. Abel Gwanafyo, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wakati akikagua hatua za ujenzi wa Meli Mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu”, jijini Mwanza.

Ameongeza kuwa hadi kufikia sasa Serikali tayari imemlipa mkandarasi zaidi ya asilimia 70 na kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha hizo na kwamba kwa sasa kazi ya ujenzi wa meli hiyo inaendelea vizuri.

Aidha, Mhandisi Kasekenya amesema kuwa meli hiyo itakapokamilika itafungua fursa za kiuchumi na kibiashara kati ya jiji la wa Mwanza, mikoa jirani ya Musoma, Bukoba kupitia Bandari ya Kemondo Bay pamoja na nchi jirani za Uganda na Kenya. Muonekano wa Meli Mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” inayojengwa jijini Mwanza ambayo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 53.8 na itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 magari madogo 20, magari makubwa 3 pamoja na mizigo tani 400. (PICHA ZOTE NA WUU).

Naye, Kaimu Meneja wa Bandari ya Ziwa Victoria, Bw. Vicent Steven, amemueleza Naibu Waziri Kasekenya kuwa tayari TPA imeshafanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kupanua na kuboresha miundombinu ya maegesho yote yatakayopokea meli hiyo na kwamba kwa sasa wako kwenye hatua za manunuzi yatakayo wezesha kumpata mkandarasi atakayeifanya kazi hiyo.

Meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” inajengwa na wakandarasi kutoka kampuni ya GAS Entec Company na KANGNAM Corporation za Korea Kusini na itakapokamilika inatarajiwa kuwa na madaraja sita (6) yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200, magari madogo 20, magari makubwa 3 pamoja na mizigo tani 400 na hivyo inatarajiwa kuwa meli kubwa kuliko zote katika Ziwa Victoria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news