TUGHE yapata viongozi wapya Taifa, Joel Kaminyonge ndiye Mwenyekiti

Na Rotary Haule,Dodoma

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania ( TUGHE ) kimefanikiwa kupata safu mpya ya viongozi watakaokiongoza chama hicho katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mwenyekiti mpya wa TUGHE Taifa, Joel Kaminyoge akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kwake mjini Dodoma. (Picha na Rotary Haule).

Viongozi hao wamechaguliwa kufuatia uchaguzi wake mkuu uliofanyika Septemba 29, mwaka huu Mjini Dodoma.

Katika uchaguzi huo nafasi ya uenyekiti iligombewa na watu watatu akiwemo Pacience Bachuba, lakini ushindani mkali ulikuwa baina ya aliyekuwa akitetea nafasi yake, Archie Mntambo na Joel Kaminyoge .

Katika uchaguzi huo msimamizi wa uchaguzi Andrew Mwalwisi,alimtangaza Joel Kaminyoge kuwa mwenyekiti wa Taifa wa TUGHE kwa kupata kura 147 na kumwangusha aliyekuwa akitetea nafasi hiyo Archie Mntambo aliyepata kura 80 kati ya kura halali 243 .

Mwalwisi alisema nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na Jane Madete aliyepata kura 143 dhidi ya Peruth Gwasa aliyepata kura 101 Kati ya kura 244 zilizopigwa.

Nafasi ya Katibu Mkuu wa TUGHE aliyeshinda ni Hery Mkunda aliyekuwa akitetea nafasi yake na hatahivyo hakuwa na mpinzani na hivyo wajumbe kupiga kura ya ndiyo au hapana ambapo Mkunda alishinda kwa kura 185 huku 47 zikimkataa.

Nafasi ya Vijana ilikuwa na wagombea watatu akiwemo Dominices Nyoni ,Juma Nyamuhanga na Paul Maige lakini Nyoni ameibuka kidedea kwa kupata kura 138 na kuwabwaga wenzake wawili .

Mwalwisi,alisema kwa upande wa nafasi ya mwakilishi wa walemavu aliyeshinda ni John Kabeho aliyepata kura 124 huku Neema Mpombo akipata kura 83 kati ya kura 207 za wajumbe wote.

Alisema kuwa pamoja na matokeo hayo lakini bado uchaguzi huo utaendelea kufanyika kwa nafasi nyingine mbalimbali ikiwemo ya kuwapata manaibu Katibu wakuu wawili.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi mwenyekiti wa TUGHE Taifa Joel Kaminyoge ,aliwashukuru wajumbe kwa namna walivyojitoa kumchagua yeye na viongozi wengine wa chama.

Kaminyoge ,alisema kuwa uongozi ulioingia madarakani utakwenda kuhakikisha unaanzisha miradi ya kimkakati itakayosaidia kuongeza mapato ya chama.

Alisema kuwa, haiwezekani kusubiri ada za wanachama kwa ajili ya kuendesha chama jambo ambalo ni ngumu na kwamba lazima wafike sehemu washirikiane katika kukijenga chama.

"Tunawashukuru kwa kutuamini na sisi tunasema mtu baadae chama kwanza na tutakwenda kuleta mabadiliko makubwa ya kimafanikio ndani ya chama chetu kwahiyo tunaomba ushirikiano kutoka kwenu wajumbe", alisema Kaminyoge

Hatahivyo, Kaminyoge alisema wataongoza chama kwa mujibu wa sheria ,taratibu na kwa misingi ya katiba yao huku akisema pamoja na mambo yote hayo lakini lazima wafanyekazi kwa kuheshimu mamlaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news