NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa umelalamikia vitendo vya kishirikina vinavyofanywa hospitalini hapo.
Hali hiyo inatajwa kuhatarisha usalama kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo na kuzua hofu.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Martha Chacha ameyabainisha hayo wakati akitoa taarifa kwenye kikao kazi kilichojumuisha wataalamu,viongozi wa ngazi ya jamii na wakunga wa jadi leo.
Amedai kuwa, hali iliyopo sasa inatisha ambapo watendaji wa hospitali hiyo wamekuwa wakitishwa na mauza mauza yaliyopo katika hospitali hiyo hasa nyakati za usiku.
Mganga huyo amesema kuwa, vitendo hivyo vya kishirikina vimekuwa vikififisha ari ya kufanya kazi kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo kwa maana ya wauguzi, manesi na wengineo wawapo zamu za usiku.
Pia anasema, ukwamishwa kufanya kazi zao kwa kukumbana na mauza uza kama vile kuvutwa miguu na kitu kisichoonekana,kuzima taa na kuziwasha wakiwa wanatoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa.
Mganga huyo amesema kuwa, watumishi wengi wa hospitali hiyo ukataa kupangwa zamu za usiku na kuifanya kazi yao kuwa ngumu kiasi cha wengine kufikiria kuomba uhamisho kwenda kufanya kazi katika maeneo mengine.
Hivyo amewaomba wazee wa eneo hilo kukaa na kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa haraka ili waendelee kutoa huduma kwa jamii katika hospitali hiyo.
Pia amewataka wananchi kuendelea kuitumia hospitali hiyo ya wilaya na kudai kuwa toka waanze kutoa huduma kwa muda wa mwaka mmoja sasa kasi ya wagonjwa wanaokwenda kupata huduma katika hospitali hiyo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya wagonjwa waliopo.
Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi wa hospitali hiyo, Crementina Kaishozi kwa upande wake amewataka wakunga wa jadi kuacha mara moja kuwazalisha akina mama wajawazito bali kazi yao iwe ni kuwasindikiza wateja wao hospitalini.
Pia amesema kuwa, sasa hivi maisha yamebadilika sana na magonjwa ni mengi hivyo si wakati mzuri sana kwao kuendelea kuzalisha akina mama, hospitali ndiyo mahala sahihi na wao kuwa mabalozi katika maeneo yao ya kueleza umuhimu wa Mama mjamzito kujifungulia hospitalini.
Diwani wa Kata ya Isunta, Isaac Chambula na Kudra Hamad wa Kata ya Kipundu walikerwa na taarifa hiyo ya kishirikina na kuutaka uongozi wa hospitali hiyo ya wilaya kuitisha viongozi wa dini kwenda kufanya maombi katika hospitali hiyo ili kuweza kukabiliana na vitendo hivyo vya kishirikina.