WACHIMBAJI KUNUFAIKA NA OFISI MPYA YA GST GEITA -WAZIRI BITEKO

Na Steven Nyamiti- WM

WACHIMBAJI wa madini Kanda ya Ziwa na maeneo ya jirani wametakiwa kutumia huduma za utafiti, ushauri elekezi, uchambuzi wa sampuli katika maabara ili wachimbe kwa tija.
Waziri wa Madini,Doto Biteko akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa jengo la Kituo cha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) iliyofanyika tarehe 21 Septemba, 2021 mkoani Geita.

Rai hiyo, imetolewa na Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Septemba 21, 2021 wakati akifungua jengo la Kituo cha Ofisi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) mkoani Geita kwa ajili ya kutolea huduma.

Waziri Biteko amesema, utafutaji wa madini ni sayansi, hivyo wachimbaji watumie sayansi katika kutafuta madini.

"Tuwatumie wataalam ambao nchi imewasomesha kwa gharama kubwa ili waweze kusaidia kupata taarifa sahihi za miamba na uwepo wa madini katika maeneo tunayofanyia kazi," amesema Waziri Biteko.

Amesema, GST imeona ni muhimu kusogeza huduma ya ofisi karibu na maeneo ya wachimbaji na watendaji.

"Nataka niwahakikishieni, tukio hili ni mwanzo wa mambo mengi ambayo Sekta ya Madini itafanya kwenye Mkoa wa Geita," ameongeza Waziri Biteko.

Kwa upande mwingine, Waziri Biteko amesema, ujenzi wa jengo la kisasa lenye thamani ya shilingi bilioni 4 na milioni 500 unaanza hivi karibuni ili huduma zitolewe karibu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila akizungumza wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Kituo cha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) iliyofanyika tarehe 21 Septemba, 2021 mkoani Geita.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema, Serikali na Wizara ya Madini imekuwa ikiwezesha sana GST ili iweze kuimarisha miundombinu ya kutoa huduma yao.

Prof. Msanjila amesema, kusogeza Kituo cha GST katika Mkoa wa Geita unalenga kuwawezesha wachimbaji katika kuchangia kikamilifu Pato la Taifa.

Mtendaji Mkuu wa GST, Musa Budeba, amesema, ofisi ndogo iliyozinduliwa na Waziri Biteko pamoja na ofisi zitakazojengwa sehemu mbalimbali zitatoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kama vile namna ya uchukuaji sampuli ili kuwajengea uwezo wa kuchimba kwa tija.
Mtendaji Mkuu wa GST, Dkt. Mussa Budeba akizungumza wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Kituo cha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) iliyofanyika tarehe 21 Septemba, 2021 mkoani Geita.

"Pia kutoa ushauri elekezi kwa wadau wa Sekta ya Madini kwa gharama nafuu, kufanya utafiti wa kina wa jiosayansi katika kanda ili kubaini sehemu zenye viashiria wa uwepo wa madini, na kuuza na kusambaza machapisho ya ramani, taarifa na vitabu mbalimbali vya taarifa ya GST," ameeleza Budeba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya GST, Prof. Justinian Ikunguru amesema, ofisi ya GST iliyozinduliwa inakwenda kutimiza ndoto ya GST ya kuwa na ofisi za kanda ili kusogeza huduma za taasisi karibu na wadau wa Sekta ya Madini.
Mbunge wa Jimbo la Geita Joseph Musukuma, akizungumza wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Kituo cha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) iliyofanyika tarehe 21 Septemba, 2021 mkoani Geita.
Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Costantine Kanyasu, akizungumza wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Kituo cha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) iliyofanyika tarehe 21 Septemba, 2021 mkoani Geita.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Madini Doto Biteko na wadau wa Sekta ya Madini wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Kituo cha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) iliyofanyika tarehe 21 Septemba, 2021 mkoani Geita.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule, ameipongeza Serikali na wizara kwa kuanzia ofisi ya kanda katika Mkoa wa Geita ambayo itakuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo.

Jengo la Kituo cha GST mkoani Geita limefunguliwa rasmi na Waziri Biteko na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news