Na Steven Nyamiti-WM
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imewataka wachimbaji kutumia Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini kujifunza teknolojia mbalimbali zilizopo kwenye maonesho yaliyoanza leo Mkoani Geita.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa kwenye banda la STAMICO walipotembelea Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yaliyoanza leo katika Viwanja vya Maonesho Bombambili EPZ Mkoani Geita leo Septemba 16, 2021.
Wito huo umetolewa leo Septemba 16, 2021 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Seif Gulamali alipotembelea banda la Wizara ya Madini na taasisi zake katika Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yaliyoanza leo Septemba 16, 2021 katika Uwanja wa Bombambili EPZ.
Amewataka wachimbaji na wafanyabiashara kutumia fursa hiyo ya teknolojia mbalimbali ambayo Wizara na Serikali imeandaa kupitia maonesho ili kuwaonyesha wananchi shughuli zinazofanyika katika Sekta ya Madini.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Seif Gulamali akizungumza alipotembelea Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yaliyoanza leo katika Viwanja vya Maonesho Bombambili EPZ Mkoani Geita leo Septemba 16, 2021.
Kuhusu madhara yanayopatikana kutokana na matumizi ya Zebaki katika kukamatia madini ya dhahabu, Gulamali amesema, kuna umuhimu wa Serikali ya mkoa, wizara au wadau kuhakikisha wanatoa misaada mbalimbali katika kuwezesha huduma za kijamii kwa jamii zinazozunguka migodi ili kusaidia kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa wa saratani.
"Tuchangie katika kuboresha huduma ya saratani kwa sababu wagonjwa wa Kanda ya Ziwa upata huduma katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es salaam. Ni umbali mrefu zaidi ya kilomita 1,000 kufika huko, huduma ya saratani ikisogezwa karibu itasaidia kutoa huduma,"amesema Gulamali.
Pia, Gulamali amesisitiza wadau mbalimbali kusaidia Hospitali ya Rufaa ya Bugando ili kukamilisha ujenzi ili wagonjwa wa saratani wapate matibabu katika hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amesema, lengo la maonesho ni kuonesha teknolojia zinazotumika katika Sekta ya Madini.
Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya akizungumza kwenye Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanaliyoanza leo katika Viwanja vya Maonesho Bombambili EPZ Mkoani Geita leo Septemba 16, 2021.
"Tunapokutana wadau wengi tunabadilishana uzoefu kwa wale wanaochimba bila kujua teknolojia nyingine rahisi wanaweza kutumia maonesho haya kujifunza,"amesema Prof. Manya.
Aidha, Prof. Manya amesema kuwa, Wizara ya Madini inatambua mchango wa Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini katika kubadilishana uzoefu.
"Maonesho ya Teknolojia ya Madini Wachimbaji Wakubwa wanaweza kuwapa uzoefu wachimbaji wadogo na wale wachimbaji wa kati,"amesisitiza Prof. Manya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amewahamasisha wananchi wa Kanda ya Ziwa na Geita kutumia fursa kubwa zilizopo katika Uwanja wa Maonesho kwa muda wa siku 10.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akizungumza kwenye Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanaliyoanza leo katika Viwanja vya Maonesho Bombambili EPZ Mkoani Geita leo Septemba 16, 2021.
Amesema, kupitia maonesho hayo wadau watapata elimu, kuunganishwa na wafanyabiashara, kupata ujuzi mpya, watapata vifaa vya kisasa vinavyoendana na uchimbaji wa madini, uchenjuaji na uzalishaji wa madini.
Pia, Senyamule ameeleza kuwa Maonesho ya Nne ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yatafunguliwa Rashmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa tarehe 22 Septemba 2021. Maonesho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu ya "Sekta ya Madini kwa Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu".