Na Dotto Mwaibale, Singida
WATU 50 waliokuwa wamelazwa Hospitali ya Mkoa wa Singida wakipatiwa matibabu baada ya kunusurika kufa baada ya kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya afya zao kuimarika.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Binilith Mahenge alipowatembelea wananchi hao Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Banuba Deogratius amesema walipokea jumla ya wagonjwa 50, wanawake 34 na wanaume 16 ambapo hali hadi leo hali zao zilikuwa zikiendelea vizuri na baadhi yao wameanza kuwaruhusu kurudi nyumbani kuendelea na majukumu yao ya ujenzi wa Taifa.
Banuba amesema, wakazi hao wa Kata ya Unyambwa Kijiji cha Kisasida katika Manispaa ya Singida mkoani hapa walifikishwa hospitalini hapo baada ya hali zao kuwa mbaya kutokana na kula chakula kilichoandaliwa katika shughuli za ufunguzi wa Madrasa moja katika kijiji hicho.
Akipokea taarifa hiyo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Bilinith Mahenge amewapongeza madaktari wa hospitali hiyo kwa jitihada walizozifanya za kuhakikisha wananusuru maisha ya wananchi hao ambapo kwa sasa hali zao zinaendelea vizuri na kuipongeza Serikali kwa kuweka miundombinu mizuri ya huduma katika sekta ya afya.
Ametoa wito kwa viongozi wa Serikali na dini kuwajibika kikamilifu katika kutoa elimu ya namna ya kuandaa chakula pamoja na kusimamia inapotokea sherehe mbalimbali kwenye maeneo yao ili kuepuka madhara ya namna hiyo yasije kutokea tena.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi, ASP Stella Mutabihirwa amesema wanawashikilia watu saba kuhusika na tukio hilo.
Amesema, katika tukio hilo mtoto mmoja mwenye umri wa miaka saba aliyemtaja kwa jina la Fahad Masoud alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.