Watumishi watatu wa Afya wadakwa wizi wa mashine ya kuangalia mapigo ya moyo, upumuaji hospitali

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Siku moja baada ya DIRAMAKINI Blog kuripoti kuhusu wizi wa mashine ya kuangalia Mapigo ya Moyo, Upumuaji, Wingi wa hewa ya Oksijeni katika damu kwa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji katika chumba cha upasuaji mkubwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu tayari Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia watumishi watatu wa Idara ya Afya kwa tuhuma za wizi huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Richard Abwao ameeleza kuwa, uchunguzi katika eneo la tukio (hospitali) ulibaini kuwa chumba hicho cha upasuaji hakikuvunjwa.

"Mnamo tarehe 20/09/2021 majira ya saa 07:30 asubuhi huko Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Simiyu (Nyaumata), iliyopo mtaa wa Nyaumata, Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, Getrude Emmanuel (45), msukuma, mkristo na katibu wa hospitali ya mkoa Simiyu, aligundua kuibiwa kwa mashine 01 inayojulikana kwa jina la Cadiac Monitor Accessories yenye namba za usajili ex-7c051585 yenye thamani ya sh. milioni 7,820,000 iliyokuwa kwenye chumba cha kufanyia upasuaji wa macho.

"Kiini cha tukio hili ni kujipatia kipato kisicho halali, wafanyakazi katika chumba hicho cha upasuaji wamekamatwa na wanahojiwa kuhusiana na tukio hili ni Paul Igosha (37), msukuma, mkazi wa Somanda, Neema Msekile (24), mnyakyusa, mkazi wa Kidinda na Edward Yirika (27), muha, mkazi wa somanda ambao wote ni wauguzi katika chumba cha upasuaji wa macho Hospitali ya Nyaumata,’’amesema.

Kamanda Abwao ameeleza kuwa, baada ya tukio hilo kuripotiwa kituoni hapo upelelezi mkali ulianza mara moja kwa kukagua eneo la tukio na kuhoji baadhi ya mashahidi na baada ya mahojiano hayo timu hiyo ya makachero waliwakamata watumishi wa chumba cha upasuaji wa hospatali hiyo ambao ni Paul Igosha, Neema Msekile na Edward Yirika ambao walihojiwa lakini walikana kuhusika na tukio hilo.

Amesema, tarehe 22/09/2021 majira ya saa 09:0hrs alikamatwa Allen Cosmas (30), Daktari wa usingizi, chumba cha upasuaji ambaye pia alihojiwa na makachero na hatimaye kukiri kuhusika na tukio hilo, ambapo alieleza kuwa mashine hiyo ameuza mkoani Mwanza.

Ameongeza kuwa,timu hiyo ya makachero ilielekea mkoani Mwanza eneo la kona ya Bwiru Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza na kufanikiwa kumkamata rafiki wa Daktari huyo aitwaye Enord Iginatio Kalekezi (29), Daktari kituo cha afya Kisorya wilayani Bunda mkoani Mara, ambaye alihojiwa na kueleza kuwa ameuza kwa Daktari aitwaye David Omollo (32), Daktari wa hospitali binafsi iitwayo Royal Hospital iliyopo kona ya Bwiru wilaya ya mkoa wa Mwanza.Soma kisa kamili hapa>>>

Amesema,timu ya makachero ilifika hospitalini hapo na kufanikiwa kuikamata mashine hiyo iliyokuwa kwenye chumba cha upasuaji hospitalini hapo (Royal Hospital) na tayari imeshaletwa na imeifadhiwa Kituo cha Polisi Bariadi kama kielelezo.

Ameongeza kuwa, mpaka sasa watuhumiwa watatu ambao ni Allen Cosmas, David Omollo na Edward Ignatio wapo mahabusu kituo cha polisi Bariadi kwa mahojiano na baada ya mahojiano kukamilika watafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news