Na Tito Mselem-WM
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitaka Idara ya Madini wizarani kwake inayosimamiwa na Kamishna wa Madini nchini, Dkt. Abdul-Rahman Mwanga kuwa na maono na uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza jambo wakati wa kikao baina yake na watumishi wa Idara ya Madini leo, kulia kwake ni Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Utawala na usimamizi wa Rasilimali Watu, Issa Nchasi.
Ameitaka idara hiyo kuelewa kuwa ipo juu ya taasisi zote zilizo chini ya wizara na kuwa ndiyo moyo wa wizara na kwamba ni idara pekee iliyobeba Wizara ya Madini na hivyo inapaswa kujiongoza na kuwa taarifa za kutosha zinazohusiana na sekta.
Waziri Biteko ameeleza hayo leo alipokutana na watendaji wa Idara ya Madini katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa wizara uliopo Mji wa Magufuli jijini Dodoma ambapo idara hiyo imepata Kamishna Mpya mara baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Akizungumzia lengo la kikao hicho, Waziri Biteko amesema na kueleza matarajio waliyonayo kama wizara kwa idara hiyo na kuwataka wajipange katika kufikia matarajio ya kuendelea kuifanya Sekta ya Madini kuwa kinara katika kukuza uchumi wa Taifa.
Akitoa maelekezo ya majukumu wanayopaswa kutekelezwa na idara hiyo, Waziri Biteko ameitaka idara hiyo kufuatilia kwa ukaribu suala la kuhuisha Sera ya Madini ya Mwaka 2009 iliyolenga katika kufungamanisha uchumi wa madini na sekta nyingine za kiuchumi nakubainisha kuwa sera hiyo imepitwa na wakati.
Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Usimamizi wa Mazingira, Mhandisi Gilay Shamika akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya idara yao na Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani).
Biteko ameongeza kuwa, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 iliyoweka mkazo katika suala la ushiriki wa nchi na wananchi katika uchumi wa madini ambapo Rais ndiye msimamizi mkuu wa Madini kwa niaba ya wananchi Sera iliyopo haiongelei chochote kuhusu marekebisho ya Sheria hiyo.
Akizungumzia utekelezaji wa majukumu kwa sehemu (sections) zilizo chini ya Idara hiyo, Waziri Biteko amewataka wasimamizi na watendaji katika sehemu hizo kujituma katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria na kutongoja kupangiwa kazi ndipo watekeleze. “Vitu vya kufanya ni vingi mno, mbadili mfumo wa kutekeleza majukumu yenu na kila mmoja wenu awe na uelewa wa nini anakwenda kutekeleza kwa siku husika uwapo kazini” amesisitiza Biteko.
Aidha, Waziri Biteko amemtaka Kamishna wa Madini kushirikiana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika kuhakikisha kinaeleza mazuri yanayofanywa na wizara kwa umma ili kuwapa uelewa wa sekta wadau na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza katika kikao hicho Kaimu Katibu Mkuu, na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Issa Nchasi ameitaka Idara ya Madini kuupitia na kuwasilisha mapendekezo ya Muundo wa idara yao endapo wataona inafaa kufanyia marekebisho maana una miaka minne tangu uanze kufanya kazi.
Pamoja na hayo, Nchasi amewataka maafisa walioko masomoni kutumia nafasi hiyo ya masomo kutafiti juu ya masuala yanayohusiana na Sekta ya Madini ili kuja na maoni yatakayoongeza tija katika utendaji na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. “Lengo kuu la kuwapeleka chuoni sio vyeti bali tunahitaji mfanye tafiti zitakazoinua Sekta ya Madini ili itoke ilipo na kukua zaidi” anakazia Nchasi.
Waziri wa Madini Doto Biteko (mbele kulia) akiendelea na kikao na watumishi wa Idara ya Madini alipokutana nao kuweka mambo ya kiutendaji sawa mara baada ya uteuzi wa Kamishna mpya wa Madini Dkt. Abdul-Rahman Mwanga
Kwa upande wake, Kamishna Mteule wa Madini, Dkt. Abdul-Rahman Mwanga amemhakikishia Waziri na watumishi anaowasimamia kuwapa ushirikiano wa kutosha na kuwafanya kufurahia mahali pa kazi.
Dkt. Mwanga amewataka maafisa anaowasimamia kuwa na ratiba ya utekelezaji wa majukumu ya idara kwa kila mmoja pasipo kujali uwepo wa pesa ili inapowezekana majukumu waliyojipangia yaweze kutekelezwa kwa wakati muafaka kuliko kupanga majukumu mara baada ya kupokea fedha jambo litakaloondoa ufanisi katika utendaji wao.
Aidha, Kamishna Dkt. Mwanga amebainisha kuwa, kama idara wana jukumu kubwa la kubaini changamoto zinazozikabili taasisi zilizo chini ya wizara na kumshauri Waziri namna ya kutatua changamoto hizo na kuahidi atafanya hivyo kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha wizara inafanya vizuri katika kukuza uchumi wa madini.