Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameitaka Taasisi ya SHELTER AFRIQUE kuratibu maonesho ya Kimataifa ya Dunia ya Teknolojia na ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu nchini Tanzania.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akizungumza wakati wa kikao na Taasisi ya Shelter Afrique kujadili mikakati ya kusadia maendeleo ya makazi na teknolojia bora ya ujenzi wa nyumba bora za gharama leo tarehe 3 Septemba 2021 jijini Dodoma. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi mteandaji wa Shelter Afrique Andrew Chimphondah, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo.
Waziri Lukuvi alitoa kauli hiyo leo tarehe 3 Septemba 2021 alipokutana na ujumbe wa taasisi hiyo katika ofisi za wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma uliokwenda kwa ajili ya kuelezea mikakati yake kwa ajili ya kutangaza mikakati yake katika kusaidia ujenzi na teknolojia rahisi ya ujenzi kwa nchi wanachama.
Lukuvi amesema, Serikali iko tayari kutoa eneo kwa ajili ya kufanyika maonesho hayo kwa kushirikisha makampuni mbalimbali Duniani aliyoyaeleza kuwa yataisaidia kutangazwa kwa teknolojia za ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu na hivyo kusaidia wananchi na makampuni yanayofanya kazi za ujenzi.
Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mteandaji wa Shelter Afrique, Andrew Chimphondah akizungumza wakati wa kikao na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kujadili mikakati ya taasisi yake kusaidia maendeleo ya makazi na teknolojia ya ujenzi wa nyumba bora za gharama nchini leo tarehe 3 Septemba 2021 jijini Dodoma.
‘’Tunataka Shelter Afrique mratibu maonesho na wadau wengine duniani kwa ajili ya kuonesha teknolojia mpya au teknolojia nyingine kwa ajili ya ujenzi wa nyumba bora na gharama nafuu na maonesho hayo yawe ya kidunia,"amesema Lukuvi.
Shelter Afrique ni Taasisi ya kifedha yenye nchi wanachama 44 Barani Afrika inayosaidia maendeleo ya ujenzi kwenye sekta ya nyumba na maendeleo ya mijini nchini Afrika ambapo hutoa bidhaa na mikopo ya fedha kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba bora za makazi kwa gharama nafuu.
Amesema, serikali iko tayari kutoa eneo la ekari hamsini kwa ajili ya kufanyika maonesho hayo kila mwaka na kubainisha kuwa maonesho hayo yahusishe teknolojia rahisi ya ujenzi wa nyumba bora na vifaa vya ujenzi kwa lengo la kutoa elimu kwa makampuni ya ujenzi na wananchi kuweza kumudu gharama za ujenzi.
Kwa Tanzania Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuwa katika jitihada kubwa za kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya kuuza na kupangisha ambapo kwa sasa shirika hilo linaendesha miradi yake maeneo ya Iyumbu na Chamwino mkoani Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, viongozi wa Wizara na wale wa Taasisi ya Shelter Afrique wakifuatilia uwasilishwaji taarifa mikakati ya Shelter Afrique kusadia maendeleo ya makazi na teknolojia bora ya ujenzi wa nyumba bora za gharama leo tarehe 3 Septemba jijini Dodoma.
Sehemu ya ujumbe wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukifuatilia maelezo ya Waziri wa Ardhi William Lukuvi wakati wa kujadili mikakati ya kusadia maendeleo ya makazi na teknolojia ya ujenzi wa nyumba bora za gharama leo tarehe 3 Septemba 2021 jijini Dodoma.
‘’NHC kwa ina kiwanda cha kutengeneza matofali, eneo kwa ajili ya kuchimba kokoto na pia tunajenga kiwanda kwa ajili ya kutengeneza zege na tuko mbioni kuwa na kiwanda cha mabati na tutaanza kwa kazi za ndani za shirika,"amesema Mkurugenzi wa Ujenzi wa NHC Mhandisi Hekamen Mlekio.
Waziri Lukuvi ameihakikishia taasisi ya Shelter Afrique kuwa yuko tayari kuishawishi serikali kutekeleza miradi yake kupitia teknolojia itakayotangazwa au kuonesha kuwa ni bora na ya gharama nafuu.
Kwa mujibu wa Lukuvi, Serikali ya Tanzania iko tayari pia kutoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa nyumba na kusissitiza kuwa bado Tanzania inayo ardhi kubwa kwa ajili ya uwekezaji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara na wale wa Taasisi ya Shelter Afrique baada ya kikao cha pamoja cha kujadili mikakati ya Shelter Afrique kusadia maendeleo ya makazi na teknolojia ya ujenzi wa nyumba bora za gharama leo tarehe 3 Septemba jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
akisisitiza jambo wakati wa kikao na Taasisi ya Shelter Afrique kujadili
mikakati ya kusadia maendeleo ya makazi na teknolojia bora ya ujenzi wa
nyumba bora za gharama leo tarehe 3 Septemba 2021 jijini Dodoma.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Shelter Afrique, Andrew Chimphondah ameishukuru wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ushirikiano mkubwa inaounesha kwa taasisi hiyo ikiwemo kutoa michango yake na kueleza kuwa, uamuzi wa kukutana na nchi wanachama kama Tanzania ni jitihada za kutekeleza azimio la Younde (Younde Declaration).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo aliishukuru taasisi ya Shelter Afrique kwa kuelezea mikakati yake kwa wizara hiyo na kueleza kuwa ana imani ushirikiano baina ya wizara na taasisi hiyo utaleta matokeo chanya katika masuala ya ujenzi wa makazi bora.