NA MWANDISHI MAALUM
Jana nimefanya ziara fupi kwenye Kituo cha Udhibiti wa Mfumo wa Usafirishaji Umeme (Grid Control Center - GCC), Ubungo, Dar es Salaam. Ziara hii haikuwa sehemu ya Mpango Kazi wa Miezi Sita niliojipangia bali ni kutokana na malalamiko ya wananchi wengi kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara katika siku, wiki na miezi ya hivi karibuni.TANESCO wametoa sababu nyingi za kadhia hii. Lakini nimebaini mambo manne:-1. TANESCO haina mfumo wa kiteknolojia wa kubaini kwa haraka ukatikaji wa umeme kwenye maeneo mengi ya mitaani (yaliyo katika mfumo wa usambazaji).2. Wananchi wengi wanakosa namna ya uhakika ya kuripoti kukatika kwa umeme au changamoto nyinginezo ikiwemo kuunganishiwa umeme, na hata pale wanapoweza, hawapati majibu fasaha au majawabu huchelewa kupatikana.3. Taarifa za awali (advance notice) za kuzimwa kwa umeme katika maeneo kadhaa kutokana na matengenezo yaliyopangwa (planned mantainance), hazipelekwi kwa ufanisi kwa wananchi walio wengi. Hivyo, kupelekea kukosekana kwa maandalizi na hivyo kuongeza malalamiko.4. Kwa muda mrefu, matengenezo ya kawaida (repair and maintenance) ya miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme yamekuwa hayafanyiki kwa kiwango stahiki na hivyo kupelekea miundombinu kuwa chakavu na kusababisha kadhia ya sasa ya kukatika kwa umeme mara kwa mara. Mwaka jana, kwenye repair and mantainace ya miundombinu ya usafirishaji na usambazaji, TANESCO ilipanga kutumia shilingi bilioni 80.5 (ambayo bado ni chini ya kiwango cha kimataifa ki-asilimia ya mapato ya Shirika). Hata hivyo, kiwango kilichotumika ni shilingi bilioni 67 tu.Ili kukabiliana na kadhia ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, nimeelekeza TANESCO kama ifuatavyo:-1. Kuhakikisha kwamba tatizo hili, hasa pale kunapotokana na uzembe na ucheleweshaji wa matengenezo, linaisha ndani ya wiki mbili. Zaidi ya hapo, tutalazimika kuwaondoa kazini wahusika.2. Kuimarisha mfumo wa huduma kwa wateja, ikiwemo kuweka mfumo wa kiteknolojia wa kupokea na kutoa taarifa, kwa wakati na kwa ufasaha, kwa wananchi.3. Viongozi wa Shirika kutokimbia wajibu wa kuwasiliana na umma kuhusu changamoto za huduma ya umeme na kutegemea wanasiasa wawasemee. Kwahiyo, kuanzia Jumatatu, tarehe 20/09/2021, kwa wiki nzima, wawakilishi wa Shirika wajitokeze kwenye vipindi vya moja kwa moja vya vyombo vya habari mbalimbali vya habari na kupokea kero za wateja wao kuhusu huduma ya umeme na kuzitolea majawabu.4. Kuhakikisha kwamba matengenezo na maboresho yanayopaswa kufanywa kwenye mfumo wa usafirishaji na usambazaji, ili kuondoa vifaa chakavu, yanafanyika bila kucheleweshwa. Na Wizara ipatiwe repair na maintenance plan.Pamoja na kwamba sikuwa nimepanga kufanya ziara hii kwa wakati huu, nilichukua fursa hii kuwajulisha wafanyakazi wa TANESCO niliozungumza nao kwamba mabadiliko makubwa yanakuja ndani ya Shirika. Mabadiliko hayo yanaweza kuja na machungu, lakini ni uchungu wa uzazi – unaoishia kwenye furaha. Niliwajulisha kwamba tunawaamini na kuthamini na kutegemea utalaam wao katika uendeshaji wa Shirika hili nyeti.Tunataka kuipeleka TANESCO kwenye ngazi ya kuwa moja ya mashirika yenye thamani kubwa na yanayoheshimika zaidi Afrika Mashariki na Kati. TANESCO ina mapato ya mwaka ya takribani shilingi trilioni 1.8 – zaidi ya shirika au kampuni yoyote ile nchini, ama ya umma au binafsi. Lakini pia matumizi yake ni trilioni 1.8 – na ina deni linalokaribia shilingi trilioni moja. Ni shirika lenye mali nyingi – za thamani ya shilingi trilioni 13 - kuliko karibu kampuni yoyote nchini. Kwa assets hizi, na mapato haya, TANESCO haipaswi kusuasua kama ilivyo sasa. Asilimia 88 ya mapato ya TANESCO (shilingi trilioni 1.6) inatokana na mauzo ya umeme, kwa wateja milioni 3.2 tu. Inawezekana kabisa kutengeneza wateja wapya mara tatu ya hawa. Asilimia 23 ya gharama za TANESCO (shilingi bilioni 412) ni gharama za uchakavu wa mitambo na miundombinu (depreciation).Kutokana na uchakavu wa mitambo na miundombinu, TANESCO mwaka jana ilipoteza asilimia 16 ya umeme iliosafirisha. Kiwango cha umeme kinachoruhusiwa kupotea kimataifa ni asilimia 5. Kwahiyo, mwaka jana, tulipoteza zaidi ya asilimia 10 ya umeme tuliosafirisha – sawa na takribani Megawati 120, umeme unaotosha kuhudumia mikoa zaidi ya nane (Iringa, Njombe, Ruvuma, Tabora, Manyara, Singida, Lindi, na Mtwara).Kwa kifupi, kuna masuala mengi ya kuyapitia,ikiwemo namna ambavyo manunuzi yanafanyika. Jambo la msingi ni kwamba tutaliboresha Shirika kwa namna ambayo itawaweka juu na kuwapa thamani kubwa wateja na wafanyakazi wa Shirika. Wafanyakazi ni rasilimali muhimu katika utendaji wa Shirika. Tunataka wawe na ari mpya na kwamba hatutafokeana kama watoto wadogo na kwamba utalaamu wao utaheshimiwa bali uzembe hautavumiliwa. Tutapata siku maalumu ya kuzungumza na wafanyakazi na viongozi wote wa TANESCO na kuelezea kwa kirefu zaidi haya niliyoyagusia hapa, pamoja kuwapa muongozo, dira na mwelekeo mpya.January Makamba (MB)Waziri wa Nishati