Waziri Mchengerwa ateua wajumbe wa bodi katika tasisi mbili

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) amefanya uteuzi wa wajumbe wa bodi za taasisi mbili zilizopo chini ya ofisi yake.
Uteuzi huo unakuja, kufuatia kukamilika kwa uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bi. Sophia Elias Kaduma na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Bw.Florence M.Turuka uliofanywa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 2, 2021 kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu-Utumishi, Mheshimiwa Dkt.Laurean J.P.Ndumbaro.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu 29 (1) (b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) amefanya uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kama ifuatavyo;

"Bwana Mbaraka Mohammed Abdulwakil ambaye ni Katibu Mkuu mstaafu, Jaji Crecencia William Makuru ambaye ni Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bibi Riziki Joseph Kuhanwa ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo mstaafu wa Ofisi ya Rais na mwingine ni Kamishina Said Abeid Kamugisha ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria mstaafu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo kuhusiana na walioteuliwa.

Wakati huo huo, kwa mujibu wa taarifa hiyo,kwa mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Wakala za Serikali, Sura 245, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) amefanya uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya Chuo cha Utumishi wa Umma kama ifuatavyo;

"Jaji Awadh Mohamed Bawaziri ambaye ni Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Profesa Masoud Hadi Muruke ambaye ni Mhandisi Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,"imeongeza taarifa hiyo.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi wa wajumbe hao utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia leo Septemba 2, 2021.

"Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inatoa pongezi kwa wajumbe walioteuliwa na inawatakia kazi njema katika utekelezaji wa majukumu yao,"imefafanua taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news