Waziri Mchengerwa atoa angalizo kuhusu wimbi la matapeli

Na James K. Mwanamyoto, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewatahadharisha watumishi wa umma, wastaafu na wananchi kuwa makini na matapeli wanaotumia simu za viganjani kujipatia fedha kwa ulaghai kwa lengo la kuwasaidia katika masuala ya kiutumishi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 3, 2021 jijini Dar es Salaam juu ya utapeli unaofanywa kwa watumishi wa umma na wastaafu. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utawala wa Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amesema matapeli hao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi mbalimbali wa kiserikali na kisiasa kwa kuwapigia simu watumishi wa umma na wastaafu na kuwataka watoe taarifa zao za kiutumishi ili wawasaidie kuwapandisha madaraja, kuwateuwa kwenye nafasi za uongozi, kuwapatia ajira na masuala mengine ya kiutumishi.

Mhe. Mchengerewa amewataka wananchi na wadau wote wa masuala ya kiutumishi kuacha kutoa taarifa zozote zinazoombwa na mtu yeyote kwa njia ya simu kwani Serikali inao utaratibu wa kuwasiliana na wadau wake pindi inapohitaji taarifa za kiutumishi kwa ajili ya kuzifanyia kazi.

“Kutoa taarifa kiholela si vizuri kwani zinaweza kutumika visivyo na kumsababishia matatizo aliyetoa taarifa hizo,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo jijini Dar es Salaam juu ya utapeli unaofanywa kwa watumishi wa umma na wastaafu.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, yawezekana matapeli hao wanapata fursa ya kufanya uhalifu huo kutokana na baadhi ya viongozi na watendaji kutofikika kiurahisi pindi wadau wanapohitaji huduma, hivyo amewataka Viongozi na Watendaji hao kuacha urasimu usiokuwa na tija.

Katika kusogeza huduma karibu na wananchi, Mhe. Mchengerwa amewataka wadau ambao wanahitaji ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi kupiga simu namba 026-216-0240 ya kituo cha mawasiliano (Call Centre) cha ofisi yake na namba 026-2160-210 ya kituo cha mawasiliano cha Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Mkurugenzi wa Utawala wa Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam juu ya utapeli unaofanywa kwa watumishi wa umma na wastaafu.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi na wadau wa masuala ya kitumishi kutoa taarifa za matapeli kwenye ofisi yake na vyombo vya dola ili zisaidie kukabiliana na tatizo hilo.

Mhe. Mchengerwa ametoa onyo kali kwa matapeli hao kwani Serikali kupitia vyombo vya dola inaendelea kufuatilia nyendo zao ili kuwabaini na hatimaye kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news