Tito Mselem na Nuru Mwasampeta, WM-Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema, kuna fursa mbalimbali za uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini iliyoambatana na mazingira rafiki na salama kwa wawekezaji kuwekeza pesa zao.
Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati), Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya (kulia) na Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Preashon wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kikao kilichofanyika Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.
Ameyasema hayo alipokutana na Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Preashon aliyeambatana na Makamu Balozi kwa lengo la kujitambulisha kwa Waziri wa Madini na kueleza machache kuhusiana na uhusiano wa kisekta baina ya Tanzania na India.
Amesema, wizara inatambua uwezo wa India katika masuala ya Uongezaji Thamani Madini na kutoa mwaliko endapo watakuwa tayari kuwekeza katika eneo hilo na maeneo mengine yenye fursa katika Sekta ya Madini wasisite kufanya hivyo.
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akizungumza jambo kwenye kikao hicho na kushoto ni Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya, Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.
Waziri Biteko amemsihi Balozi Binaya kufika ofisini kwake wakati wowote endapo kutakuwa na jambo la kujadiliana katika kuboresha utendaji wa Sekta pamoja na kujadili maeneo ya ushirikiano kama atakavyoona inafaa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya aliupongeza uamuzi wa Balozi huyo wa kukutana na viongozi wa wizara na kueleza kuwa kuna maeneo tofautitofauti ya kuwekeza katika Sekta ya Madini nchini.
Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia) akiwa na Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya (kushoto) wakufuatilia kikao Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Prof. Manya amebainisha kuwa wizara inatarajia kuanza kwa mradi wa uchimbaji wa madini ya graphite yatakayoongeza fursa ya uwekezaji katika Sekta ya Viwanda nchini.
Aliongeza kuwa, Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali na kuna fursa kubwa ya kuwekeza katika viwanda kutokana na uwepo wa madini mbalimbali ya viwanda yanayoweza kutumika katika kutengenezea saruji, gypsum board, mawe ya nakshi (tiles) na vifaa vingine vya ujenzi.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao cha Waziri wa Madini Doto Biteko Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.
Aidha, Balozi wa India nchini Tanzania amebainisha nia ya nchi yake kuimarisha ushirikiano katika Nyanja za tekinolojia, elimu na biashara, pia ameshukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata.
Baadaye Waziri Biteko alikutana na uongozi wa juu wa Mgodi wa almasi Petra Diamond Tanzania ya mkoani Shinyanga na Kampuni inayojulikana kama ASN Limited na kushauriana nao namna bora ya kutekeleza majukumu yao katika maeneo yao ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima.